VIDEO: Ahsante Mzee Majuto


Neno ‘Ahsante’ ndilo pekee analostahili kuambiwa mfalme wa vichekesho nchini, Amri Athuman maarufu Mzee Majuto. Mwonekano wa sura yake tu vilitosha kuijaza tabasamu sura yako na  vichekesho vyake viliwavunja mbavu za Watanzania kwa miaka mingi. Kama ucheshi unatibu maradhi, basi Mzee Majuto ameponya wengi.
Mzee Majuto ambaye amehitimisha safari yake hapa duniani juzi, alitumia zaidi ya miaka 40 kuwachekesha Watanzania katika majukwaa, sebule na vyombo vya usafiri.
Unawezaje kupanda mabasi yanayokwenda masafa marefu na usifurahie safari yako zinapowekwa filamu alizocheza Mzee Majuto?
Kabla ya umauti, alizushiwa kifo mara kadhaa na kauli yake ya mwisho alipozungumza na mwandishi wetu, Rhobi Chacha Juni 22 alizungumzia hilo akisema, “Mwambieni huyo anayetaka nife bado napumua, asiniharakishe safari yangu bado haijafika.”
Mbali na kuchekesha, Mzee Majuto amechangia mabadiliko kwenye tasnia ya sanaa nchini kwa kuibua vipaji na kuwa mfano wa kuigwa kwa kuishi  maisha ya kawaida yasiyotawaliwa na kashfa kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wenye majina makubwa nchini.
Filamu za kuvunja mbavu alizocheza kama Sharobaro, Gumzo, Nakwenda kwa Mwanangu, Inye Gwedegwede, Mzee wa Chabo, Daladala, Swaga, Nyumba Nne na Mshamba, ni kielelezo cha mchango wake katika kuichekesha Tanzania.
Baada ya kupokea taarifa za msiba huo jana, Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliandika katika ukurasa wake wa Instagram: “Ahsante King Majuto kwa kuitendea haki tasnia ya filamu, kwa kuwapa burudani mamilioni ya wapenda filamu nchini na nje ya nchi na kwa kutufundisha wanadamu thawabu ya kicheko kupitia maigizo yako na tabasamu lililokuwa usoni kwako daima. Mwenyezi Mungu aiweke roho yako pema peponi. Amina.”
Mwanamuziki Ambene Yessaya maarufu AY pia amendika katika ukurasa wake wa Instagram: “Ahsante sana kwa kushare na sisi kipaji chako hakika tulikufurahia tangu wengine tukiwa watoto.”

Mwaka mmoja wa kuugua
Kwa zaidi ya mwaka mmoja jina la Mzee Majuto lilitawala vyombo vya habari likihusishwa na ugonjwa wa henia na baadaye tezi dume.
Taarifa za kuugua kwake ziliripotiwa Julai mwaka jana na mkewe Aisha Yusuf ambaye alisema marehemu Mzee Majuto alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo tangu Mei.
Januari, Mzee Majuto ambaye pia alijulikana kwa jina la King Majuto alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, kidonda cha upasuaji wa henia kiliendelea kumsumbua na alilazwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo katikati ya Aprili.
Serikali iliamua kumpeleka India Mei 4 kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Apollo, New Delhi na alirejea Juni 23 na moja kwa moja alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uangalizi kabla ya kuruhusiwa na kisha kurudishwa tena hospitalini hapo Julai 31 ambako alilazwa hadi kifo chake.

Mamia wamuaga
Jana, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakary Zubeiry aliongoza dua ya kumuombea marehemu katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam kabla ya mwili wa marehemu kusafirishwa kwenda Tanga kwa mazishi leo.
Rais John Magufuli aliongoza mamia ya waombolezaji waliojitokeza kumuaga msanii huyo mkongwe katika ukumbi huo. Wengine waliohudhuria ni Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Dk Mwakyembe na naibu wake, Juliana Shonza, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo.
Mbali ya viongozi hao na wengine, pia walikuwapo wasanii wa fani mbalimbali akiwamo Diamond Platnumz, Nisha, Steve Nyerere, Cloud 112 pamoja na ndugu jamaa na marafiki.
Kabla ya kupelekwa Karimjee, mwili wake uliswaliwa katika msikiti wa Maamur, Upanga Dar es Salaam.