SIMBA WAZEE WA KULIAMSHA

Wednesday August 8 2018

 


Achana na rekodi za kuwa klabu ya kwanza kuvaa jezi, viatu nchini ama kumiliki gari ama kuwazawadiwa nyota wake magari, Simba pia ina rekodi nyingine tamu ya kuwa timu yenye bahati ya kunyakua kila taji jipya likianzishwa.
Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Ligi ya Soka Tanzania (sasa Ligi Kuu Bara) ikifanya hivyo mwaka 1965. Klabu hiyo ilibeba bila kutoka jasho baada ya watani zao Yanga kususia mechi yao iliyovunjika dakika ya 80, huku wakiwa mbele kwa bao 1-0 na Chama cha Soka (FAT) kuamuru urudiwe na Vijana wa Jangwani kuingia mitini na Simba kupewa taji.
Simba ililitetea taji hilo kipindi hicho ikitumia jina la Sunderland kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Simba mwaka 1971. Klabu sita pekee ndizo zilizoasisi Ligi Kuu ya sasa ambazo ni Tobacco au Sigara (Pwani), Young African, Coastal Union na Manchester United (Tanga), TPC (Moshi) na mabingwa  Sunderland (Pwani).
Pia Simba ndiyo klabu ya kwanza kubeba taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame) ikifanya hivyo mwaka 1974.
Kama haitoshi imelibeba pia taji la Tusker lilioasisiwa mwaka 2001 na kulitetea kwa miaka mingine miwili mfululizo, kadhalika ilikuwa ya kwanza kubeba taji la michuani ya  BancABCSuper8   iliyofanyika mara mmoja tu na kuzimika 2012.
Lakini pia hata Simba Day ndilo Tamasha la kwanza kwa klabu za soka nchini, mbali na Simba pia kuwa ya kwanza kuelekea katika Mfumo wa Hisa ikiwapiga bao watani zao Yanga.

KIMATAIFA ZAIDI
Licha ya Yanga kuwa klabu ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania na kufika robo fainali kwa miaka miwili mfululizo 1969 na 1970, lakini Simba ndiyo yenye rekodi tamu katika mechi za kimataifa.
Simba ndio klabu ya kwanza Tanzania kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (enzi hizo Klabu Bingwa Afrika) 1974, pia ni klabu pekee ya Bongo kufika fainali za michuano ya Afrika ikifanya hivyo kwenye Kombe la CAF 1993.
Simba ilipoteza 2-0 nyumbani mbele ya Stella Abidjan baada ya suluhu ya mechi ya ugenini nchini Ivory Coast, pia ndio klabu pekee nchini kuwahi kumvua taji mtetezi wa Afrika ikifanya hivyo 2003 kwa Zamalek ya Misri na kutinga makundi.
Simba ndio timu pekee ya Tanzania inayowatetemesha klabu kutoka Ukanda wa Afrika Kaskazini maarufu kama Waarabu kwani imekuwa ikizinyanyasa hasa zikija Tanzania.
Klabu nyingine ikiwamo Yanga zimekuwa zikitaabika na miaka ya hivi karibuni ikiwa ni zaidi ya miaka 30 Jangwani ilijikomboa mbele ya Al Ahly ya Misri, Mo Bejaiya na MC Alger za Algeria, japo ilichapika ilipoenda kupambana nao ugenini.

KIPIGO KIKALI
Ni kweli Yanga ndio klabu ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani wa jadi nchini ikiisulubu Simba mabao 5-0 mnamo Juni 1, 1968, ila inateseka na kipigo cha paka mwizi.
Simba ililipa kisasi na kuandikisha rekodi inatowatesa Yanga kwa miaka zaidi ya 40 walipoitandika mabao 6-0 Julai 19, 1977 ikishuhudiwa King Abdallah Kibadeni akipiga hat trick.
Kama haitoshi wakati Yanga ikipambana kutaka kufuta aibu hiyo wakati ikitimiza miaka 35, iliongezewa tena dozi kwa kukadnikwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya Mei 6, 2012.
Kama unataka kuwakera Wanayanga we kumbushia vipigo hivyo vya paka mwizi ilivyopewa timu yao na wapinzani wao wa jadi ambao kwa msimu huu wanaonekana kuwa moto kweli.

MATAJI KIBAO
Ukiondoa mataji 19 iliyonayo katika Ligi Kuu Bara ikiwa nyuma ya Yanga iliyotwaa mara 27, Simba pia ina mataji mengine lukuki yanayoifanya itishe kwa klabu za Tanzania.
Katika Ligi, Simba ilibeba mataji yake 19 katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2009-10, 2011-12, 2017-2018.
Katika Kombe la Kagame Simba inashikilia rekodi ya kubeba mataji mengi ikifanya hivyo mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
Simba pia inashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Tusker mara nyingi zaidi kwa klabu za Afrika Mashariki ikifanya hivyo mara nne 2001, 2002, 2003 na 2005.
Katika Ligi Kuu ya Muungano pia ilimenyakua jumla ya mataji  sita ikifanya hivyo mwaka 1993, 1994, 1995, 2001, na 2002, huku katika Kombe la Nyerere (sasa FA) imenyakua mara nne, miaka ya 1984, 1995, 2000 na 2017.
Jumla ya mataji hayo ni 38 hapo hayajawekwa ya Kombe la CCM ama Kombe la Mapinduzi na kwa rekodi hizo tamu kwa nini wasiitwe 'Taifa Kubwa' a.k.a Wazee wa kuliamsha dude?!
0000

Advertisement