MAONI: Hongereni Simba, miaka 10 sio mchezo sasa ongezeni thamani Simba Day

Wednesday August 8 2018

 

MASHABIKI wa Simba na wadau wao wengine leo wanahitimisha Tamasha lao la Simba linalotimiza miaka 10 tangu kuasisiwa kwake mwaka 2009.
Tamasha hili liliasisiwa chini ya uongozi wa Hassan Dalali aliyekuwa Mwenyekiti na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguga ambaye ndiye haswa anayetajwa kutoa wazo hilo kwa wenzake kama kina Seydou Rubeya, Mohammed Mjenga, Chano Almas na wengineo na kuunwa mkono na kuanzishwa rasmi mwaka huo.
Asili ya tamasha hilo ilikuwa kukutanisha wadau wa Simba kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ya klabu yao sambamba na kupanga mikakati mipya kwa msimu mpya wa ligi kabla ya kuboreshwa na kuwa lilivyo sasa.
Kwa sasa tamasha hilo uanzia kila Agosti 1-8 litakaloendana na shughuli mbalimbali za kijamii kabla ya kuhitimishwa kwa burudani ya muziki na mechi ya soka inayohusisha kikosi kipya cha msimu dhidi ya timu alikwa.
Kwa mwaka huu tamasha hilo linafanyika ikiwa Simba mpya imetokea kambini Uturuki katika kambi ya wiki mbili, kitu kinachoongeza hamu kwa mashabiki wa klabu hiyo kuhudhuria kutaka kuwaona vijana wao watafanya nini msimu huu.
Tofauti na misimu mingine ya tamasha hilo, safari hii Simba imewaleta Asante Kotoko Mabingwa wa zamani wa Afrika ili kunogesha tamasha hilo, kitu ambacho kitakuwa ni kipimo tosha kwa vijana hao wa Msimbazi na Kocha Mkuu wao.
Mwanaspoti tunaipongeza Simba kuendelea kuwa klabu ya kuanzisha mambo na wengine kufuata nyuma yao, kwani suala la klabu kuwa na siku yao ni Wekundu wa Msimbazi ndio walioasisi na klabu nyingine kama Ndanda na Coastal nao kuiga.
Hili ni jambo la kujivunia kwa wanasimba kwa kuwa mfano kwa wenzao, kwani tamasha kama hilo lina thamani kubwa kwa Wanamsimbazi kuliko inayochukuliwa na ingependeza klabu nyingi zaidi zitafuata nyayo hizo.
Hata hivyo bado tunaamini Simba wanaweza kuliboresha zaidi tamasha lao la Simba Day hasa katika kulifanya liwe la kisasa zaidi na kuisaidia timu yao.
Badala Simba Day kuhitimishwa kwa mechi moja ya utambulisho wa wahezaji wapya wa kikosi hicho, ni vyema tamasha hilo likatengenezwa hata ligi ndogo ambayo ingeendeshwa ndani ya wiki nzima ya tamasha hilo kabla ya hitimisho.
Simba ingeweza kuzialika timu kubwa kutoka nchi jirani na waalikwa wengine na kuchezwa ligi ndogo kama Arsenal inavyopendeshwa michuano yao ya Emirates na mwisho mshindi anyakue taji la ligi hiyo ambapo licha ya kuisaidia timu yao, lakini pia klabu inaweza kutengeneza mapato ya ziada.
Kuwepo kwa ligi ya aina hiyo kunaweza kushawishi wadhamini kadhaa kujitokeza na hivyo kuingia fedha na mwisho kuifanya timu iimarike na pia kuwapa burudani ya kusisimua wanachama na mashabiki wa klabu yao katika Simba Day yenyewe.
Inawezekana kuna woga kwamba kuendeshwa kwa ligi ndogo ya aina hiyo kutaitibulia timu kama itakwama njiani na kuziacha timu pinzani kubeba taji au kucheza mechi ya mwisho, lakini hilo ni tamasha hivyo matokeo yoyote kwao ni kipimo cha namna gani timu ilivyo imara ama dhaifu kabla ya kuanza kwa msimu.
Ndio maana tunasema Tamasha la Simba Day bado linahitajia kuboreshwa zaidi ya inavyoendeshwa sasa, licha ya kwamba Wanasimba wanalifurahia kwa vile wanapata burudani na kutambulishwa kikosi na hata uzi mpya wa msimu.
Soka kwa sasa ni biashara inayolipa na Simba lazima waitumie fursa ya ukubwa wa jina lao, kwa kuamini kuwa ndani ya wiki nzima ya tamasha hilo Simba inaweza kuzalisha mamilioni ya fedha kuliko kusubiri kuuza jezi siku chache kabla ya mechi ya kuhitimisha tamasha hilo ama viiingilio vya mechi ya Simba Day tu.
Ndani ya wiki wakati klabu ikicheza ligi ndogo ya Simba Day, pia klabu inaweza kuuza bidhaa mbalimbali zitokanazo na klabu hiyo zikiwa na nembo ama jina au rangi ya jezi za klabu hiyo kama jezi, skafu, kalenda, vikombe, vifungulia chuma na bidhaa nyingine na kwa wingi wa mashabiki wa Simba wangevuna kiasi gani.
Ukichukua mapato ya mauzo ya bidhaa na vifaa hivyo vya Simba na yale ya viingilio vya mechi zitakazochezwa katika ligi ndogo na hata fedha wa wadhamini, klabu lazima itakuwa imenufaika ndani ya wiki ya tamasha hilo. Hilo ndilo soka la kisasa.
Ndio maana wakati tunaipongeza Simba kuingia mwaka wa 10 wa tamasha lao, lakini pia tunawakumbusha kuangalia mbele zaidi ili Simba Day lilipe nje ndani na kuifanya Simba iendelee kuwa 'Taifa Kubwa' na la kuigwa ndani na nje ya Tanzania. 

Advertisement