Stand United kunoa makali kwa Mwadui

Tuesday August 7 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Stand United kwa mara ya kwanza watashuka uwanjani Jumamosi hii kuwakabili jirani zao Mwadui FC katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu.

Timu hiyo ya mjini Shinyanga inatarajia kufungua pazia ya Ligi Kuu Agosti 22 kwa kuwakaribisha African Lyon, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema watacheza mechi hiyo kuona makali yao dhidi ya Mwadui FC Jumamosi ya wiki hii.

Alisema baada ya mchezo huo wanahitaji kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu wawe wamecheza mechi nyingine tatu ili kukiweka fiti kikosi chao na kwamba wamejiandaa vyema.

“Hadi sasa hatujacheza mchezo wowote wa kirafiki na hii ni kwa sababu tulikuwa tunajiandaa vyema, kwahiyo mchezo wetu wa kwanza tutacheza Jumamosi dhidi ya Mwadui kuona makali ya vijana wetu”alisema Billo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ellyson Maheja alisema uongozi umejipanga kutoa sapoti na motisha kwa timu yao kuhakikisha msimu huu wanafanya vizuri.

“Tunachotaka ni kumaliza Ligi katika nafasi nzuri, uongozi umejipanga kutoa aina yoyote ya sapoti,msimu uliopita japo tulifanya vizuri, lakini tunahitaji msimu huu tuzidi hapo”alisema Maheja.

 

Advertisement