Kabwili atoweka Yanga, Kakolanya arejea kambini

Tuesday August 7 2018

 

By Khatimu Naheka

Morogoro. Kipa chipukizi Yanga, Ramadhan Kabwili hadi sasa ameshindwa kujiunga na kambi ya timu hiyo Morogoro bila ya taarifa yoyote, wakati mwenzake  Benno Kakolanya amerudi kambini hapo.

Uongozi wa Yanga hauna taarifa ya sababu za Kabwili kushindwa kufika kambini mapema jambo lililosababisha katika mazoezi ya jana jioni mshambuliaji Amissi Tambwe atumike kama kipa.

Habari njema kwa Yanga ni kurejea kwa Kakolanya aliyekuwa katika kumaliza msiba wa kaka yake uliotokea kwao Mkoani Mbeya.

Kipa huyo alijiunga na timu hiyo jana jioni ambapo leo asubuhi alikuwa katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Chuo cha Mapadri kilichopo Bigwa nje kidogo ya Mkoa wa Morogoro.

Kurejea kwa kipa huyo kumemfanya kocha wa makipa kuwa na makipa wawili katika mazoezi ya leo kufuatia jana kuwa na kipa mmoja pekee Mkongomani Klause Kindoki.

Kindoki alionekana jana kuwa pekeyake na kuifanya Yanga kumtumia mshambuliaji Amissi Tambwe kuwa kipa wa pili.

 

Advertisement