Mambo saba yaliyomvuta kocha mpya Mnigeria

Dar es Salaam. Mambo saba muhimu yamelivutia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumteua mshambuliaji nyota wa zamani wa Nigeria ‘Super Eagle’, Emmanuel Amunike kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’

Kiwango cha elimu ya ukocha, uzoefu kwenye taaluma hiyo, mafanikio kwa timu alizofundisha, uwezo wa kusaka vipaji vya soka, uwezo wa kufanya tathmini ya mchezo, ukubwa wa klabu alizocheza na mafanikio aliyopata akiwa mchezaji ni vipaumbele muhimu ambavyo vimeishawishi TFF kumpa nafasi hiyo kujaza nafasi ya Salum Mayanga.

Hadi anateuliwa kuwa kocha wa Taifa Stars, Amunike aliyewahi kucheza Barcelona, ana shahada ya uzamili ya ukocha kutoka Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), pia ana Leseni A ya ukocha.

Kiwango hicho cha elimu kimemfanya Amunike kupata nafasi ya kuwa kocha kwenye timu takribani 10 tofauti katika kipindi cha miaka 14 alichofanya kazi kwenye taaluma hiyo tangu alipostaafu rasmi soka mwaka 2004.

Baada ya kustaafu, Amunike alifundisha timu ya vijana ya S.D Reocin ya Hispania kwa mwaka mmoja na mwaka uliofuata alikinoa kikosi cha wakubwa kabla ya kutimkia Saudi Arabia alikokwenda kufundisha Al-Hazm Club.

Mwaka 2008 alirejea Nigeria kuifundisha Julius Berger alikodumu kwa mwaka mmoja na baadaye alijiunga na Ocean Boys inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.

Baadaye alifundisha timu ya Taifa ya vijana ya Nigeria chini ya miaka 17 na 20. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Nigeria kabla ya kwenda Sudan kufundisha klabu ya Al-Khartoum aliyodumu nayo hadi anateuliwa Taifa Stars.

Amunike ameshinda tuzo ya Kocha Bora Afrika mwaka 2015, pia aliiongoza timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2015 na 2013.

Katika kusaka vipaji, Amunike amewahi kufanya kazi ya kuwa skauti wa Manchester United kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Pia kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2010 hadi 2013 alifanya kazi ya kuwa mchambuzi wa soka kwenye kituo cha luninga cha Al-Jazeera Sport.

Kabla ya kujihusisha na ukocha, Amunike mbali na kucheza timu tofauti za taifa Nigeria, alicheza klabu za Nigerlux, Concord na Julius Berger za Nigeria, Zamalek (Misri), Sporting Lisbon (Ureno), Barcelona, Albacete (Hispania), Pusan Icons (Korea Kusini) na Al-Wehdat (Jordan).

Mafanikio aliyopata akiwa mchezaji ni kutwaa taji la Ligi Kuu ya Nigeria mwaka 1991, Ligi ya Misri (1992,1993), Kombe la Washindi Afrika (1993), Mataifa ya Afrika (1994), Mchezaji Bora wa Afrika (1994), Kombe la Ureno, Medali ya Dhahabu ya Olimpiki (1996), Kombe la Mfalme Hispania (1997, 1998), Kombe la Washindi Ulaya (1997) na Ligi Kuu ya Hispania (1998, 1999).

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema shirikisho hilo lina imani na Amunike na wanaamini ataleta mabadiliko chanya ya timu ya Taifa na soka la Tanzania.

“Tumeingia mkataba wa miaka miwili na Amunike ambao unaweza kuboreshwa kama ataweza kutimiza tulichokubaliana. Ni mtu mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika na tumejiridhisha atakuwa msaada kwa soka letu,” alisema Karia.

Amunike alisema amekuwa akilifuatilia soka la Tanzania muda mrefu na anaamini akipata ushirikiano wa kutosha litapiga hatua.

“Nimeshawahi kuja hapa nikiwa na Zamalek lakini pia nilishawahi kuiona Taifa Stars ikicheza na Nigeria kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia. Nafahamu kiu na matarajio mliyonayo, lakini sitaki kuwa mtu wa kuahidi, naamini tukishirikiana pamoja tutafanikiwa,” alisema Amunike.

Apewe muda

Aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Amunike apewe muda kwa kuwa ni mapema kumpima kabla ya timu hiyo kucheza mechi.

“Unajua Tanzania makocha wazawa hawana thamani kama wanayopata makocha wa kigeni, ujio wa Amunike ni sawa, tumpe muda tutajua tatizo liko wapi,” alisema Rishard.

Kocha na mchambuzi wa soka Kenny Mwaisabula alisema ujio wa Amunike ni sahihi, lakini tatizo la Taifa Stars ni mfumo usiokuwa na tija.

“Anaweza kuwa ana kiwango cha kuinoa Taifa Stars au la, vyovyote vile hatuwezi kumuhukumu hivi sasa, wacha tumpe muda, lakini kama mfumo wa soka hautabadilika tutamuona hafai,” alisema Mwaisabula.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema kuwa waliomteua Amunike walivutiwa na vigezo walivyotaka, hivyo anatakiwa kupewa muda.

“Sio baada ya miezi miwili naye aonekane hafai, apewe muda afanye kazi kuijenga timu sio kazi ya wiki nne ni kazi ya muda mrefu yenye mipango iliyoshiba,” alisema Kibadeni.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema rekodi ya Amunike alipokuwa mchezaji wa Nigeria sio mbaya na ameshauri apewe muda wa kumpima uwezo wake uwanjani.

“Makocha kutoka Nigeria wamekuwa na rekodi nzuri kwa Amunike tujaribu kumpa muda tuone kama atatufikisha kwenye kiwango bora kama ilivyokuwa Nigeria katika soka la Afrika,” alisema Mayay.

Imeandaliwa na Charles Abel, Thobias Sebastian na Imani Makongoro