Tetesi za usajili Ligi Kuu hizi hapa

Tuesday July 17 2018

 

By OLIPA ASSA

TETESI za uhamisho wa wachezaji kutaka kuanza maisha kwenye timu mpya watakazozichezea  msimu unaokuja zinaendelea, wakihusihswa kufanya mazungumzo ya hapa na pale, huku wengine dili zao zikiwa zimetia tiki.
Mwanaspoti linakuletea mwendelezo wa tetesi zinazowahusu mastaa mbalimbali wa ligi kuu, wanaotaka kuvaa uzi mpya katika msimu wa 2018/19.

Aziz Sibo anukia Mbao FC
MBAO FC inaendelea kusuka kikosi chake kwa msimu ujao, chini ya kocha Amri Said na sasa inasemekana wapo katika mazungumzo ya mwisho na aliyekuwa beki wa Majimaji- Songea Aziz Sibo, ili kuimarisha eneo lao la ulinzi.
"Kifupi tunahitaji kikosi kitakachohimili wingi wa mechi zitakazokuwepo msimu ujao, kulingana na ongezeko la timu kutoka 16 mpaka 20, ndio maana tunaendelea kuwasaka wachezaji wapya," alisema mmoja wa viongozi wa Mbao.
***
Shamte arejeshwe mjini
AFRICAN Lyon iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao, imemalizana na beki wa Mbeya City, Haruna Shamte ili aweze kuitumikia timu hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka kwa mmoja wa mabosi wa Lyon, zilieleza walivutiwa na uwezo aliouonyesha nyota huyo wa zamani wa Simba kwa msimu, hivyo atawasaidia.
"Tunatumia muda na akili nyingi kuangalia wazoefu na wenye uwezo uwanjani, hivyo Shamte tunaamini ni mchezaji makini ndio maana tumemsajili," alisema.
***

Mwadui yatamani Shomary
KIRAKA Ally Shomary anachomeshwa mahindi Msimbazi, lakini Mwadui wao wanammezea mate wakimuona lulu na sasa wanataka kumdaka kwa mkopo ili awasaidie kwa msimu ujao.
Habari za ndani ya Mwadui zinasema kuwa, klabu hiyo inamtaka Shomary kwa kuona atawasaidia kwa kipai alichonacho, licha ya kushindwa kuitumikia vyema Simba msimu uliopita ikimsajili toka Mtibwa Sugar.
Shomary alipoulizwa ishu hiyo alijibu kwa kifupi: "Mie kokote freshi kwa vile kazi yangu ni kucheza soka."

Advertisement