AFC yafyeka kikosi kizima

Tuesday July 17 2018

 

By YOHANA CHALLE

MACHALII wa Arachuga hawatanii aisee, katika kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao uongozi wa  timu ya AFC Arusha wameamua kuwatema wachezaji kibao wa timu hiyo waliocheza msimu uliopita.
Katibu msaidizi wa timu hiyo, Immanuel Minja alisema wamebakiza wachezaji 10 kati ya 30 waliokuwa nao msimu uliopita hii imetokana na mahitaji na sifa alizohitaji kocha mpya, Martin Mahimbo anayetaka wachezaji wenye uwezo wa kupambana.
“Ligi ya safari hii itakuwa ngumu kutokana na mfumo wa makundi mawili ya FDL yaliyowekwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF), hivyo kila timu inatakiwa kuhakikisha inaibuka nafasi za juu na kujiweka mazingira mazuri, ndiyo maana hata sisi tunahitaji wachezaji bora,” alisems Minja.
Aliongeza timu hiyo itakuwa na kikosi cha wachezaji 25 na hadi sasa wamesajili wachezaji 12 wengi wakitoka Cosmo, Villa Squad, Coast Union, Mshikamano, Polisi Dar na Small Kids huku watatu waliosalia wapo kwenye mazungumzo ya mwisho kabla ya kusaini.
Hivi karibuni, AFC walipata uongozi mpya katika uchaguzi mkuu ambao ni mara ya kwanza kufanyika kwa zaidi ya miaka mitano baada ya viongozi wengi kuikimbia klabu hiyo kutokana na ukata uliokuwa unaikabili.

Advertisement