Mashabiki wa Simba 'wamteka' Kerr kiaina

Tuesday July 10 2018

 

By MWANDISHI WETU

KOCHA wa Gor Mahia, Dylan Kerr juzi alikuwa kivutio kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mashabiki wa Simba kumteka kiaina na kumpeleka Jukwaa Kuu eneo la VIP B na kumshangilia kwa nguvu.
Kerr alikuwa upande wa pili wa jukwaa kuu, mashabiki wa Simba walipomwona, walimwita akaruka uzio na kuwafuata huku wakimshangilia.
Kerr alikuwa uwanjani hapo kuishuhudia Simba ikicheza na AS Ports ya Djibouti ambayo Simba iliifunga bao 1-0 ikiwa ni saa chache baada ya timu yake kuilaza Vipers ya Uganda mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali ya kwanza.
Baada ya Kerr kufika kwa mashabiki hao, walimkalisha kwenye kiti na wakaanza kugombania kupiga naye selfie.
Wakati akipiga picha hizo, ghafla alisimama kuelekea upande wa wanaokaa mashabiki wa Yanga na kuonyesha kama mtu anayechinja na kuamsha kelele za mashabiki wa Simba waliokuwa wamejazana jukwaani wakimfuatilia.
Dakika chache kabla ya mchezo kuanza, mashabiki walimzonga kwa kutaka kupiga naye picha, ndipo akasimama tena na kuonyesha kama kuchinja kwa mashabiki wa Yanga na kelele zikalipuka tena huku wakisema Simba...Simba...Simba.
Baada ya kitendo hicho, Kerr alichukuliwa na mmoja wa mashabiki wa Simba ambaye yuko karibu na mmoja wa viongozi vigogo wa usajili na kupanda naye juu VIP A ambako aliishuhudia Simba ikiingia nusu fainali kwa kuitoa AS Ports.
Akizungumzia tukio hilo, Kerr alisema amefurahi kwmaba mashabiki wa Simba bado wanamkubali na haamini kama anapendwa kiasi hicho.
Kerr alisema kuwa wakati wowote yuko tayari kurudi Simba. lakini akatoa masharti watu wawili katika uongozi hataki wakiwemo.
Ukiacha Kerr kuchangamsha uwanja hasa mashabiki wa Simba, vijana wake wametinga nusu fainali kwa kuilaza Vipers ya Uganda mabao 2-1.
Mchezo huo wa robo fainali ya kwanza uliokuwa na ushindani kutoka kwa timu hizo mbili, ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufuatiwa na mchezo huo wa Simba.
Vipers ambao ni mabingwa wa Uganda, walikuwa mbele kwa bao 1-0 hadi mapumziko lililofungwa na Thadeo Lwanga dakika ya 14, baada ya kupiga shuti kali la mbali akiwa nje ya eneo la hatari.
Kipindi cha kwanza Gor Mahia ilifanya mabadiliko kwa kumwingiza winga machachari Francis Kahata anayewaniwa na Simba dakika ya 43 ambaye alibadili sura ya mchezo.
Gor Mahia ilianza kipindi cha pili kwa kasi ikishambulia lango la Vipers na mfungaji wake hodari, Jacoques Tuyisenge alifunga bao la kusawazisha dakika ya 47.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Kenya, waliongeza kasi na kupata bao la pili dakika ya 73 baada ya Jacques Tuyisenge kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Vipers kabla ya Mustapha Francis kufunga. Gor Mahia sasa inasubiri mshindi kati ya Azam FC na Rayon Sport zilizokuwa zikicheza jana.
Gor Mahia iliwakilishwa na: Boniface Oluoch, Philemon Otieno, Godfrey Walusimbi, Haron Shakava, Charles Momanyi, Ernest Wendo, Innocent Wafula, Humphrey Mieno, Jacques Tuyisenge, Francis Mustapha and George Odhiambo.

Advertisement