Ndiwa aipa Kenya medali ya fedha Jumuiya ya Madola

Monday April 9 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Mwanariadha Stacy Ndiwa amefufua matumaini ya Kenya kutamba katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayoendelea kutimua vumbi, Gold Coast, Australia, kwa kushinda medali ya fedha ikiwa ni medali ya tatu kwa Kenya.

Ndiwa alimaliza akiwa wa pili akitumia muda wa dakika 31:46:36, katika mbio za mita 10,000 kwa wanawake, zilizofanyika mapema leo na kuiongezea Kenya medali nyingine katika kapu lake.

Mwanariadha huyo wa Kenya alipata ushindani mkali kutoka kwa Waganda Stella Chesang aliyemaliza wakwanza akitumia dakika 31:45:30,huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mganda mwengine, Mercyline Chelagat aliyemaliza mbio hizo ndani ya dakika 31:48.41.

Beatrice Mutai ambaye alikuwa anapigiwa upatu kuipeperusha bendera ya Kenya, alimaliza katika nafasi ya nne, akitumia dakika kushinda who was also a medal 31:49.81.

Mkenya mwengine katika mbio hizo alikuwa ni Sandrafelis Chebet, ambaye tofauti na matarajio ya wengi, alijikuta akimaliza katika nafasi ya kumi (32:11:92), licha ya kuweka rekodi ya kuandikisha muda wake bora katika mashindano makubwa.

Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo Waethiopia, wamekuwa wapinzani wakuu wa Kenya katika mbio ndefu, katika makala haya ya 21 ya mashindano ya Jumuiya ya Madola, Kenya imejikuta ikiburuzwa vibaya na wanariadha wa Uganda.