Azam: Kombe haliendi Uganda

Thursday January 11 2018

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. AZAM FC imeutaja mchezo wake wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda keshokutwa Jumamosi kama wa vita katika kujenga heshima ya Tanzania kwa kuhakikisha Kombe hilo linabaki nchini.

Timu hizo mbili zimefanikiwa kuingia fainali baada ya kuibuka na ushindi katika hatua ya nusu fainali iliyochezwa jana ambapo Azam FC iliwatoa Singida United kwa bao 1-0 wakati URA iliiondoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4.

Afisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Iddi alisema Azam FC haiko tayari kuruhusu kombe hilo kuondoka nje ya ardhi ya Tanzania kutokana na heshima na thamani ya Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar.

"Sasa Watanzania lazima waamke, hasa wa Tanzania Bara na Visiwani vilevile. Azam sasa inawakilisha nchi na sio yenyewe peke yake. Tayari Simba wameshatoka, Yanga wameshatoka na Singida nao pia wameshatoka. Kwa Azam ndio waliobakia wanacheza na Uganda.

Kama inacheza na Uganda tunaomba sapoti ya Watanzania. Maana sasa hivi umekuwa mchezo wa kimataifa tena na sio kombe la Mapinduzi, kati ya Uganda. Tunaelekea katika mapambano makubwa kati ya Uganda na Tanzania hivyo tunaomba Watanzania watuunge mkono na tutahakikisha hatuwaangushi," alisema Iddi.