Mbaya wa Yanga ambwaga Bocco Tuzo za TFF

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Mbao FC, Habibu Kiyombo aliyeifunga Yanga mabao mawili peke yake walipokutana kwenye mechi ya Ligi Kuu, Desemba 31 amechaguliwa  mchezaji bora wa mwezi Desemba mwaka jana.

Kayombo alifunga mabao hayo wakati timu yake ilipoifunga Yanga 2-0, kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Amechaguliwa baada ya kuwashinda straika wa Simba,  John Bocco 'Adebayor' na beki wa Azam FC Bruce Kangwa.

Kiyombo amepita baada ya kufunga mabao hayo mawili katika mechi yao na Yanga. Mabao hayo yamemfanya afikishe saba kwenye msimamo wa ligi kuu akiwa nyuma ya Emmanuel Okwi raia wa Uganda mwenye manane.

Bocco aliingia kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa Simba wa 2-0, dhidi ya Ndanda FC na  Kangwa aliisaidia Azam katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United alipofunga bao moja na kutoa pasi ya  bao lingine.

Kutokana na ushindi huo, Kiyombo atazawadiwa Tuzo maalumu, ile ya kisimbusi cha Azam na fedha taslimu Sh 1 mil kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi, Kampuni ya Vodacom.

Wachezaji wengine ambao tayari wametwaa tuzo ya mwezi kwa msimu huu ni Emmanuel Okwi wa Simba mwezi Agosti, Shafiq Batambuze waSingida kwa Septemba, Obrey Chirwa wa Yanga mwezi Oktoba na Mudathir Yahya wa Singida kwa Novemba.