Breaking News
 

Kilichowapata Yanga kwa URA ni kumbukumbu aisee!

Thursday January 11 2018

 

By THOMAS NG'ITU

UNASHANGAA Yanga kufungwa na URA penalti 5-4, kwenye Kombe la Mapinduzi, mbona hii si mara ya kwanza, ilishatokea  msimu wa mwaka juzi wa 2016.

Jana Jumatano, Yanga iliondolewa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na URA ya Uganda ambayo imefudhu kucheza fainali na watakutana na Azam FC.

Hii ni mara ya pili na kwa lugha nyingine unaweza kusema, Yanga ni wateja wa URA kutokana na matokeo  hayo, tena kwa staili hiyo ya kufungana kwa penalti hatua ya nusu fainali.

Mwaka juzi, Yanga iliondolewa kwa penalti 4-3, baada ya kumaliza kwa sare ya 1-1, mabao yakifungwa na Mrundi Amiss Tambwe kwa Yanga na Peter Lwisa kwa URA wakaenda fainali na kuchukua ubingwa.

Penalti za mwaka huo zilipigwa na Geofrey Mwashiuya na Malimi Busungu wakakosa na waliopata ni Kelvin Yondani ‘Vidic’, Deogratius Munish ‘Dida’ na Simon Msuva kwa upande wa Yanga na URA zilipigwa ni Jean Kulaba, Said Kyenune, Deogratius Othieno na Brian Mwete wakapata wakati Sam Ekito alikosa.

Na mwaka huu, Straika Mzambia Obrey Chirwa ndiyo aliiua Yanga baada ya kupiga penalty ya mwisho na kukosa, waliopiga wakapata ni Mkongo Papy Tshishimbi, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, Raphael Daud na Gadiel Michael.