Penalti ya Chirwa gumzo

Thursday January 11 2018

 

By Thobias Sebastian

Zanzibar. Shujaa aliyetegemewa kuleta heshima kwa Yanga kuipeleka fainali ya Kombe la Mapinduzi, Obrey Chirwa amepeleka kilio makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Chirwa amegeuka shubiri kwa mashabiki wa Yanga baada ya kukosa penalti ya mwisho dhidi ya URA ya Uganda katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Hata hivyo, penalti hiyo ya Chirwa imezua mjadala baada ya picha ya video kuonyesha kuwa kipa wa URA alitoka mapema golini hivyo penalti ilipaswa kurudiwa mwamuzi hakuwa sahihi kuikubali.

Kimsingi katika upigaji wa penalti, mpigaji anapewa kipaumbele kikubwa kuliko Kipa.

 Ndio maana kipa anapotokea na mpigaji akafunga, penalti haitakiwi kurudiwa ila kama akitokea na mpigaji akakosa, inapaswa kurudiwa.

Chirwa kama mpigaji wa penalti alipaswa kumpa ishara Mwamuzi kabla hajapiga kwamba Kipa ametoka.

Maana yake mwamuzi alijiridhisha kwamba utokaji wa kipa haukuwa na madhara kwa Chirwa na ndio maana hajampa ishara kwamba kipa katoka

Mshambuliaji huyo aliwasili visiwani hapa jana asubuhi kutoka Dar es Salaam baada ya kutokuwemo katika kikosi muda mrefu.

Chirwa aliyeongozana na kocha George Lwandamina, alikwenda nyumbani kwao Zambia na moja ya picha alizoweka katika mitandao kijamii ilimuonyesha akiwa analima mahindi shambani.

Mchezaji huyo alikosa penalti ya tano iliyoamua ushindi wa mabao 5-4 baada ya URA kupata penalti zote tano baada ya timu hizo kutoka suluhu dakika 90.

Penalti hiyo ilikuwa ni hitimisho la kiwango duni alichokionyesha Chirwa katika mchezo wa jana tangu alipoingia dakika ya 53.

Licha ya kwenda kwa unyonge wakati akienda kupiga mkwaju wa penalti, Chirwa alicheza chini ya kiwango na alionekana kutokuwa fiti.

 

Pambano lenyewe

Yanga ilianza mchezo ikiwa imefanya mabadiliko ya wachezaji wanne waliocheza dhidi ya Singida United ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Lwandamina aliitazama mechi hiyo akiwa jukwaani akiendelea kuwaamini wasaidizi Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila tangu kuanza kwa mashindano hayo.

 

Yanga iliwapumzisha Edward Makka, Gadiel Michael, Yohana Nkomola na Rafael Daud na nafasi zao kujazwa na Papy Tshishimbi, Juma Mahadhi,Haji Mwinyi na Said Juma 'Makapu.

Ikionekana kupania kuivunja mapema nguvu ya URA ambayo imekuwa ikitegemea zaidi safu ya kiungo, Yanga ililazimika kuanza na mfumo 4-2-3-1 tofauti na 4-4-2 ambao wamekuwa wakitumia katika idadi kubwa ya mechi walizocheza katika mashindano hayo.

Tofauti na Yanga, URA ilifanya mabadiliko mawili katika kikosi chao kilichocheza na Simba jana iliwaanzisha Ssemda Charles na Bokota Labama wakichukua nafasi za Peter Lwasa na Sseruyide Moses.

Hata hivyo, muda mrefu wa mchezo mpira ulichezwa eneo la katikati kwa kila timu kuonekana kuwa na hofu ya kutoruhusu bao la mapema.

URA ilijaribu mara kadhaa kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga, lakini ustadi wa mabeki wa timu hiyo uliisaidia kutowapa mwanya Waganda hao kupata bao.

Moja ya shambulizi ilitokea dakika ya 10 ambapo kipa Youthe Rostand alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa mkwaju wa faulo wa Brian Majwega ambao ulipatikana baada ya Haji Mwinyi kufanya madhambi.

Kitendo cha URA kumiliki mpira kwa muda mrefu, viliwalazimisha viungo wa Yanga walioongozwa na Tshishimbi kutovuka mstari unaougawa uwanja.

Dakika chache kabla ya mapumziko, Yanga ilipata mpira wa adhabu nje ya eneo la hatari, lakini shuti la Ibrahim Ajibu.

Baada ya Chirwa kuingia mwanzoni mwa kipindi cha pili, dakika chache baadaye URA iliwapumzisha Labama Bokota na Charles Sampa huku nafasi zao zikichukuliwa na Peter Lwasa na Hudu Mulikyi na dakika ya 75 Yanga ilimtoa Mahadhi na kumuingiza Yohana Nkomola.

Yanga ilijaribu kuamka na kuanza kushambuliana kwa zamu na URA lakini safu yake ya ushambuliaji ilionekana kukosa uelewano na kuwapa mwanya mabeki wa wapinzani wao kucheza kwa uhuru mkubwa.

Nusura Nkomola aipatie Yanga bao la ushindi dakika moja baadaye baada ya kupiga shuti kali nje ya eneo la hatari la URA.

Taharuki ilitokea dakika ya 81 baada ya Lwassa kuunganisha kwa kichwa mpira uliopita nyavu za nje ambazo zilikuwa zimechanika na kuingia ndani ya bao la Yanga lakini mwamuzi alikataa bao hilo jambo lililosababisha azongwe na wachezaji wa URA.

Mbali na Chirwa aliyekosa, Yanga ilifunga penalti zake nne kupitia kwa Papy Tshishimbi, Gadiel Michael, Hassan Kessy na Rafael Daud wakati penati tano za URA zilifungwa na Mbowa Patrick,Kibumba Enoch, Shafiq Kagimu, Jimmy Kulaba na Brian Majwega.

Baada ya mchezo huo, nahodha wa URA, Allan Munaaba alisema kilichowapa mafanikio hadi wakaweza kufuzu hatua ya fainali ni juhudi na nidhamu ya kufuata kile walicholekezwa.

"Tumekuja kwenye haya mashindano tukiwa na lengo la kuondoka na ubingwa na ndio maana tumekuwa tukicheza kwa bidii katika kila mchezo na hilo linaweza kujidhihirisha kwa matokeo yetu kwani tumeweza kuifunga timu inayooongoza ligi ya Tanzania, inayoshika nafasi ya pili na ile iliyopo nafasi ya nne," alisema Munaaba.

Kiungo wa Yanga, Said Juma 'Makapu' alisema timu yake ilionyesha kiwango kizuri ingawa wapinzani wao walikuwa na bahati.

"Tuliingia kwenye mchezo huu tukiwa na lengo la kutowapa nafasi ya kucheza na kutushambulia na tulifanikiwa kufanya hivyo lakini kwa bahati mbaya tukapoteza kwenye penati. Tunarudi kwenye ligi naamini tutafanya vizuri," alisema Makapu.