Ishu ya Kamusoko, Ngoma pale Yanga kumbe ipo hivi

Monday December 11 2017

 

By OLIPA ASSA

YANGA bado ipo njia panda kuamua hatma ya straika wake, Donald Ngoma, ikitatizwa pia na majeraha aliyonayo kiungo wao fundi, Thabani Kamusoko, wakati huu wanapojiandaa kwa michuano ya kimataifa mwakani.

Yanga inatarajiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ratiba ya michuano hiyo inatarajiwa kupangwa katikati ya wiki hii, ili kujua itaanza na nani, huku nyota wake hao kundi, huku Wazimbabwe hao wakiendelea kuwa majeruhi.

Majeruhi hao wamekuwa wakimpasua kichwa Kocha George Lwandamina na wasaidizi wake, akipiga hesabu ya kuimarisha kikosi chake mapema kabla ya michuano ya Afrika haijaanza, sambamba na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo Daktari wa Yanga, Edward Bavu, amefichua ishu nzima ya majeraha ya wachezaji hao na hata wa timu nyingine za Ligi Kuu ikiwamo wa watani zao, Simba.

Dokta Bavu alisema maandalizi ya wachezaji kabla ya kuanza msimu ni muhimu sana, lakini kwa bahati mbaya wachezaji wengi huwa hawayapendi na huyategea na matokeo yake ni kupata maumivu kila mara.

“Mfano mzuri ni pale Yanga ilipokwenda kujiandaa Morogoro, yale mazoezi ni muhimu sana kwa ajili ya kuandaa miili yao, saikolojia yao na mishipa ya damu kufanya kazi yake kwa ustadi,” alisema Daktari huyo.

“Chunguza kwa umakini wale waliokuwepo Morogoro, majeraha yao yanapona haraka, lakini ambao hawakuhudhuria inawachukua muda mrefu, kwani miili yao haipo tayari kufanya kazi ngumu na saikolojia zao nzito kuamua mambo,” aliongeza Bavu.

Katika mazoezi hayo ya maandalizi ya Ligi Kuu, Wazimbabwe hao walichelewa kuungana na wenzao jambo linaloelezwa kuwa ndio chanzo cha kina Kamusoko na Ngoma kushindwa kurudi mapema uwanjani.

Straika mwingine ambaye amekuwa akiikosesha raha Yanga ni Amissi Tambwe ambaye msimu huu hajacheza mechi yoyote kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti na kuifanya Yanga iwategemee Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa.

Tatizo Umri

Daktari huyo pia alifichua tatizo jingine linalochangia wachezaji wengi kuumia ni umri mkubwa.

“Mchezaji akijiona umri umeenda, lazima ajiheshimu na kujitunza, pia afanye mazoezi kabla ya mechi, wengi wao wanafanya vichekesho ili mashabiki wawaone, akiingia uwanjani tu baada ya dakika 10 anaumia,” alisema.