Mata: Ni mapema kuwapa ubingwa City

Thursday December 7 2017

 

London, England. Kiungo wa Manchester United, Juan Mata amesema bado kuna safari ndefu kuelekea kupata ubingwa, pamoja na Manchester City kuwa katika msimu mzuri.

Man City imeshinda mechi 14 na kutoka sare moja katika mechi 15 za Ligi Kuu, na kuongoza ligi kwa tofauti ya point inane mbele ya Man Utd inayoshika nafasi ya pili.

Watani hao wa jadi wa jiji la Manchester watakutana Old Trafford Jumapili hii, na Mata anaona kuna nafasi kubwa ya kupunguza tofauti hiyo ya pointi.

“Wamefanya kazi nzuri kushinda mechi nyingi”, alisema Mata kuhusu City. "Wamefunga mabao mazuri, lakini nafikiri na sisi tunaifanya vizuri kazi yetu. Tutajaribu kuwaonyesha hilo Jumapili kwa kucheza soka vizuri na kushinda na kuondoka kwa pointi tatu.

“Ni mechi ya kipekee, wote tunajua hilo, sasa wakati huu ambao timu zote zipo juu katika msimamo wa ligi.

"Tunacheza dhidi ya City kwenye Uwanja wa Old Trafford ni moja ya mechi kila moja anataka kucheza, pia ni mechi ya aina yake katika Ligi Kuu England."