Zanzibar yaaga Chalenji

Muktasari:

  • Zanzibar imetwaa ubingwa wa mashindano ya Chalenji mara mbili na awamu iliyopita pindi yalipofanyika Kenya mwaka 2017 ilishika nafasi ya pili

KIPIGO cha bao 1-0 ilichokipata mbele ya Kenya, kimeifanya timu ya taifa ya Zanzibar eroes kuaga mashindano ya Chalenji yanayoendelea jijini hapa Kampala.
Bao hilo pekee la Kenya lilifungwa katika dakika ya 48 na Oscar Wamalwa.
Wamalwa alifunga bao hilo akimalizia kwa shuti la wastani, pasi ya kupenyeza iliyopigwa na Daniel Sakari.
Mara baada ya kuingia kwa bao hilo, Zanzibar walijitahidi kusukuma mashambulizi langoni mwa Kenya ili kusaka bao la kusawazisha na la ushindi lakini safu ya ulinzi ya Kenya iliyoongozwa na beki Joash Onyango ilikuwa makini kuzuia nyavu zake zisitikiswe.
Benchi la ufundi la Zanzibar Heroes licha ya kufanya mabadiliko kadhaa katika mchezo huo, hayakuweza kuisaidia kusawazisha na kupata ushindi katika mechi hiyo.
Mabadiliko hayo ambayo yalifanywa katika kipindi cha pili ni yale ya kuwatoa Makame Abdulaziz, Abdulswamad Kassim na Zakaria Abdulmalik Adam huku nafasi zao zikichukuliwa na Mudathir Yahya, Kassim Khamis na Awesu Awesu.
Matokeo hayo yameifanya Zanzibar ibakie na pointi yake moja iliyoipata baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Sudan.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, kocha wa Zanzibar, Hemed Morocco alisema wamesikitishwa kupoteza mchezo hu na kuaga mashindano hayo.
"Ndio yameshatokea na tumeshatolewa nadhani tatizo kubwa ni kwamba wachezaji wa Zanzibar hawapati nafasi ya kutosha kushiriki mashindano ya kimataifa," alisema Morocco