Zahera awapa mastaa wake mbinu za mwisho

Muktasari:

Baada ya mtanange huo wa Kesho, Yanga watawafuata Pyramids huko Nchini Misri kwaajili ya kucheza mtanange wao wa mkondo wa pili ili kujua hatima yao ya kutinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametumia dakika 60 kuwapa maelekezo wachezaji wake kwa nadharia na vitendo huku ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea katika mtanange wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Pyramids.

Mazoezi hayo yaliyofanyika leo Jumamosi asubuhi Uwanja wa Nyamagana jijini hapa, yalianza saa 04:12 asubuhi huku kocha huyo akiondoka baada ya saa moja na kumuachia msaidizi wake Noel Mwandila alieendelea kwa dakika 30.

Katika mazoezi hayo, Zahera aliwakomalia washambuliaji wake wote kucheza mpira kwa kasi kubwa pamoja na ujanja ujanja wa kumkimbia beki wakati wakiwa na mpira huku mabeki wao akisisitiza kukaba kwa umakini mkubwa.

Katika mazoezi hayo, nyota watatu wa timu hiyo walikuwa nje wakati wenzao wakiendelea na mazoezi ambao ni Mrisho Ngassa, Raphael Daudi na beki wa kulia Paul Godfrey.

Mbali na Zahera, lakini pia Kocha wa Makipa Peter Manyika naye kwa upande wake alikomaa na makipa wake wote Ramadhan Kabwili, Metacha Mnata na Farouk  Shikhalo kudaka mipira mirefu kwa umakini mkubwa na kupooza kabla ya kuiondosha mbele.