Zahera ang’aka, atishia kuwatimua mastaa wa Yanga

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ametoa onyo kwa mchezaji atakayegoma kufanya mazoezi kujiandaa kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam unaotarajiwa kufanyika Aprili 29.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Zahera alisema mchezaji ambaye atashindwa kutokea katika mazoezi atabaki nyumbani hadi mwisho wa msimu huu.

Hata hivyo, Zahera alisema ana taarifa za wachezaji Kelvin Yondani na Papy Tshishimbi, lakini wengine waliobaki wanatakiwa kwenda uwanjani kwa mazoezi.

Kauli ya kocha huyo raia wa Congo, imekuja muda mfupi baada ya wachezaji wa Yanga jana kugoma kufanya mazoezi wakidai fedha za malimbikizo ya mishahara, pesa za usajili na posho.

Alisema katika maisha ya kufundisha soka hajawahi kuwasimamia wachezaji kama anavyofanya Yanga, lakini ameshangazwa na uamuzi waliochukua wachezaji kugoma bila ya kumpa taarifa.

“Wachezaji wa Yanga hawatapata mtu kama mimi, nimekuwa nikiwasaidia mambo mengi ndani na nje ya uwanja pamoja na maisha yao tangu nimefika Yanga. Nimesikitishwa na wachofanya bila mimi kushirikishwa.

“Baada ya kukosa mazoezi leo (jana) nimezungumza na Hafidh Saleh awaambie mtu yeyote atakayekosa mazoezi ya kesho (leo) asirudi tena kwenye kikosi changu, haiwezekani wachezaji wakaanza kugomea mazoezi mwezi mmoja kabla ya ligi kumalizika,” alisema Zahera.

Alisema suala la malimbikizo ya mishahara yao halikuanza jana na kila mmoja anatambua kuwa wanadai na ameshitushwa na uamuzi wa kugoma. Pia alitaka wachezaji waulizwe mara ya mwisho walilipwa lini mishahara yao.

Tukio la wachezaji kugoma lilitokea jana asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam walipokutana kwa ajili ya mazoezi.

Wachezaji walifika kwenye mazoezi saa 2:00 asubuhi lakini walitoa maelekezo kwa nahodha Ibrahim Ajibu na msaidizi wake Juma Abdul kumpa taarifa Zahera hawatafanya mazoezi kwa madai viongozi wamekuwa wakipuuza madali yao.

Inadaiwa wachezaji walifikia uamuzi huo baada ya viongozi wa klabu hiyo kushindwa kwenda uwanjani kama walivyokubaliana kwa ajili ya kuzungumza nao kuhusu stahiki zao.