Yussuf Poulsen afanya kweli RB

Monday February 18 2019

 

MABAO mawili ya Yussuf Poulsen mwenye asili ya Tanzania aliyofunga Jumamosi, yameendelea kuweka hai matumaini ya RB Leipzig kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’.

Poulsen alifunga mara mbili, Mercedes-Benz-Arena ambako timu yake ilikaribishwa na wenyeji wao, Stuttgart kwenye mchezo uliomalizika kwa RB Leipzig kuibuka kidedea kwa mabao 3-1.

Nyota huyo ambaye kiasili ni mtu wa Tanga, alifunga mabao hayo katika dakika ya sita na 75 kabla ya mwishoni mwa mchezo huo kupumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Matheus Santos Carneiro Da Cunha dakika ya 90.

Ushindi huo ambao RB Leipzig imeupata mbele ya vibonde, Stuttgart umeifanya kuwa na pointi 41 ambazo imezikusanya katika michezo 22 ya Bundesliga.

RB Leipzig ambayo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo iko nyuma kwa alama tisa ilizoachwa na vinara wa Bundesliga, Borussia Dortmund ambayo itacheza leo, Jumatatu dhidi ya Nürnberg.

Pia, chama la Poulsen limeachwa pointi saba na Bayern München inayoshika nafasi ya pili ikiwa na akama 48, imeachwa pointi moja na Borussia M’gladbach ambayo jana Jumapili ilikuwa na mchezo dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Advertisement