Yondani awasha moto mpyaa Jangwani

TANGU Kocha Luc Eymael atue Jangwani, beki Kelvin Yondani amekuwa na maisha magumu akichomeshwa mahindi benchi kwa madai ya utovu wa nidhamu, lakini kile alichokifanya beki huyo mkongwe mazoezini ni kama ametuma salama kwa kocha wake huyo.

Yondani ameuwasha moto mkali kwenye mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, uliopo Ubungo, Dar es Salaam akiwafunika nyota wenzake wanaojifua chini ya Kocha Msaidizi, Charles Mkwasa.

Mkongwe huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango cha juu kwa kutimiza majukumu yake ipasavyo, huku akionyesha yupo fiti kwani mazoezi yote ya nguvu ambayo Mkwasa aliwapa alifanya kwa ufanisi bila kuchoka.

Baada ya kumaliza mazoezi hayo ya nguvu, Mkwasa aliwapanga wachezaji wake katika vikosi viwili na kucheza mechi wenyewe kwa wenyewe hapo ndio Yondani alionyesha kiwango cha hali ya juu mno.

Yondani alikuwa timu ambayo inashambuliwa na mastraika kinara wa mabao wa timu hiyo, David Molinga na Yikpe Gnamien ambao hakuna hata mmoja ambaye aliweza kumpita wala kufanya hatari yoyote katika goli ambalo alikuwa analinda.

Washambuliaji hao walikuwa wakicheza kwa kushirikina kwa dakika 30 walizofanyishwa mazoezi ya kuipenya ngome iliyokuwa chini ya Yondani walikwama, kwani mkongwe huyo aliwadhibiti kwa matumizi ya nguvu, huku akiwapora mipira kiufundi na kusambaza mipira kwa wenzake.

Yondani hakuishia kuwasha moto hapo kwani, alikuwa mzuri katika mipira ya vichwa, hakuna shambulizi lolote la hatari ambalo liliweza kupita mbele yake kwani, kila shambulizi lililokuwa upande wake aliweza kuokoa au kuhakikisha timu yake inakuwa salama.

Kocha Mkwasa alimuelezea Yondani akisema kuwa, miongoni mwa wachezaji ambao wamerudi vizuri katika timu ni beki huyo kwani, ameonyesha ufanisi kwa kila zoezi alililotoa uwanjani hapo.

“Nadhani mwenyewe umeona wachezaji wengi wameonesha walikuwa wanafanya mazoezi mengi ya nguvu na kupoteza uwezo wa kumiliki mpira kwa maana wakiwa na mpira mguuni, lakini kwa Yondani amekuwa tofauti kwa hakika amefanya vizuri na kunivutia sana,” alisema.

“Huu ubora ambao ameonyesha katika mazoezi haya ya hapa ndio nitakwenda kumpatia Kocha Mkuu, kuwa Yondani amefanya vizuri kwa kila ambalo ametaka lifanyike na jukumu la kumtumia au kutofanya hivyo hilo ni lake, ila ni wazi beki huyo alikuwa makini na ametumia kipindi cha likizo kujifua vilivyo na kuwa fiti.”

Katika kikosi cha Yanga, chini ya Eymael amekuwa akiwatumia zaidi mabeki wa kati, Said Juma Makapu na Lamime Moro, huku Yondani akiishia benchi au kukaa jukwaani kama mtamazaji tu.