Yanga yavuruga nyota Namungo

Muktasari:

Mechi ya Namungo na Yanga haitakuwa rahisi kwani kwani kila upande unahitaji kupata pointi tatu ili kuzidi kujiweka kwenye mazingira salama.

MUDA mchache kabla ya Namungo kuvaana na Yanga kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara, straika wa timu wenyeji, Blaise Bigirimana amesema anatambua wanakutana na Yanga iliyotoka kufungwa na KMC, jambo litakalofanya mechi kuwa ngumu kwa upande wao.
Namungo FC kesho Jumapili itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi na  Bigirimana amesema pamoja na kwamba wao watakuwa nyumbani hawauchukulii mchezo huo kuwa rahisi kwa kutambua wageni wao watashuka wakiwa na hasira za kulipuliwa na KMC.
Nyota huyo mwenye mabao manane, amesema yeye na wenzake wanajua haitakuwa mechi rahisi kwao, lakini anaamini wana nafasi kubwa ya kuchukua pointi tatu ili kuendelea kukaa nafasi za juu.
"Tunaiheshimu Yanga ni timu ngumu ,lakini tutapambana kwa kadri tutakavyoweza ili kushinda mchezo huo, huu ni mzungu wa pili ambao kila timu ina malengo yake," amesema.
Naye Lucas Kikoti amesema watapambana kwa kadri watakavyoweza ili kuhakikisha wanawapa furaha mashabiki wao ambao watakwenda kutazama mchezo huo.
"Mechi sio rahisi ndio maana tunajipanga kuhakikisha tunapata ushindi, pointi tatu kila mchezo ni muhimu kwa sasa kwani tunaelekea mwishoni mwa ligi," amesema.