Yanga yavunja mwiko

MASHABIKI wa Yanga bado hawaamini kile kilichofanywa na nyota wao ugenini katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers, lakini kama hujui ni kwamba ushindi wa bao 1-0 iliopata Botswana imevunja mwiko kibabe.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa vijana wa Jangwani ugenini tangu mwaka juzi walipoitungua Ngaya Club de Mbe ya Comoro mabao 5-1.

Ukiondoa mechi hiyo ya Ngaya, Yanga ilikuwa ikipata matokeo ya ovyo ugenini katika michuano ya CAF kwa kupokea vipigo ama kupata sare ambapo iliwahi kupata suhulu dhidi ya Zanaco na kujikuta wakitolewa baada ya sare ya 1-1 nyumbani waliopata katika mechi ya awali.

Pia iliambulia sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya St Louis ya Shelisheli lakini wakafanikiwa kusonga mbele kufuatia awali kushinda nyumbani kwa mabao 2-0.

Mwaka jana walipoifuata Township kwao walitoka suluhu baada ya kipigo cha 2-1 nyumbani na kung’olewa ikiangukia Kombe la Shirikisho ambako licha ya kuipasua Welaita Dicha ya Ethiopia nyumbani, ilienda kulala ugenini 1-0 na kufuzu makundi.

Sio mechi za awali tu ambazo Yanga imekuwa ikiteseka ugenini hata kwenye makundi mara zote tatu ilizoshiriki ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 na Kombe la Shirikisho Afrika 2016 na 2018 haijawahi kuonja matokeo ya ushindi ugenini.

Ndipo baada ya muda mrefu, hatimaye juzi walipata ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Township na kuwavusha kwenda raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 2-1 kwani walitoka sare ya 1-1 nyumbani wiki mbili zilizopita.

Akizungumzia kuvunjwa kwa rekodi hiyo Kocha Mkuu Mwinyi Zahera alisema hatua hiyo inakuja kufuatia mabadiliko makubwa ya kikosi chao ambapo safari hii wamekuwa na timu bora ambayo inaendelea kuimarika taratibu.

“Sikuwa nafahamu kuwa, katika kipindi cha miaka miwili Yanga haikuwahi kushinda ugenini lakini ninachoweza kusema inawezekana hili inakuja wakati huu tumetengeneza timu bora kiushindani ambayo inaendelea kuimarika taratibu,” alisema kocha huyo raia wa DRC.