Yanga yamchomoa kiungo Azam FC

NGUVU na ukubwa wa Yanga, umeipa urahisi kwenye usajili wa kiungo fundi mwenye kasi uwanjani anayekipiga Prisons ambaye ni Cleophas Mkandala.

Yanga walianza kupeleka ofa lakini baadaye Azam wakaingilia na furushi la kuvutia, lakini msimamo wa Meneja wake ni kwamba; ”Utakwenda Yanga.”

Mchezaji amesema yuko tayari kucheza popote kwani timu hizo mbili ni kubwa na zina wigo mpana wa kuuza mchezaji popote.

Ameongeza kwamba anasikia jinsi vigogo hao wanavyosajili nyota wengi na kutamka kuwa hata waje 100 lakini uhakika wa namba yake uko palepale.

Licha ya kwamba dirisha la usajili halijafunguliwa, lakini timu za Simba na Yanga na Azam zimekuwa zikisaka wachezaji kwa ajili ya kujiimarisha na msimu ujao ili kufanya kweli katika mashindano yao.

Yanga imekuwa kinara kwenye uwindaji wa saini za nyota wapya, ambapo kwa sasa ni zaidi ya wachezaji wanne ambao wanatajwa kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria.

Baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa kuwa kwenye rada za Kocha Mbelgiji, Lucy Eymael ni pamoja kiungo huyo ni Zabona Khamis (Alliance) na Tuisila Kishinda wa AS Vita.

Pia wamo wengine kama Mpiana Mozizi (FC Lupopo), Bakari Mwamnyeto (Coastal Union) na Andrea Filecia anayekipiga nchini Ubelgiji katika Klabu ya Rayal Francs Borains ya Daraja la Kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkandala alisema ishu ya usajili wanaoufanya Yanga wakiwamo nyota wa kimataifa, haimshtui hata kidogo kwani anajiamini kiwango na uwezo wake.

Alisema anachojua ni kwamba dili lake likitiki huko Jangwani ushindani wa namba utakuwapo lakini anajua sehemu gani ya kuwapiku wapinzani kwani ana uwezo wa kucheza namba zaidi ya moja kulingana na mfumo wa kocha.

“Sina wasiwasi na usajili huo, hata wawepo 100 mimi sijui, ninachoamini ni uwezo wangu binafsi. Unajua wengi wana waamini wachezaji wa nje kuliko wa ndani, lakini wataona moto wangu mambo yakitiki,” alisema Mkandala.

Hata hivyo, meneja wa mchezaji huyo ambaye aliomba kutotajwa majina yake, alisema hadi sasa Yanga na Azam ndizo zimewasilisha ofa lakini kutokana na malengo ya mteja wake wanatarajia kufanya uamuzi mgumu.

Alisema Mkandala anahitaji kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, hivyo kwa timu hizo wanaona Yanga ina nafasi kubwa katika kumuweka sokoni nyota huyo kwenye medani za kimataifa.

“Kwa sasa mchezaji ameshamaliza mkataba na Prisons kilichobaki ni mechi tu, lakini ofa zilizopo ni Azam na Yanga na kutokana na malengo ya Mkandala ni kucheza soka la kulipwa nje, hivyo tumeelekeza nguvu zaidi Jangwani,” alisema meneja huyo.

Pia Meneja huyo alibainisha kuwa hata kabla ya janga la corona kuharibu hali ya hewa, nyota huyo alikuwa anasakwa na timu ya St. Luis ya Shelisheli ambayo ilikuwa imeshaleta ofa.

Kwa mujibu wa Fifa, wachezaji waliomaliza mikataba wao wanawajibika kumalizia msimu baada ya janga la corona kuathiri muda wa ligi kuisha.