Yanga yalipa kisasi kibabe

MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana waliendelea kutakata chini ya Kocha Luc Eymael, baada ya kulipa kisasi dhidi ya Ruvu Shooting kwa kuifunga bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Bao pekee la mchezo huo, liliwekwa kimiani na David Molinga katika dakika ya 40, likiwa la saba kwa straika huyo kutoka DR Congo akimalizia kwa kichwa krosi pasi ya Ditram Nchimbi.

Katika mchezo wa kwanza Yanga ikiwa wenyeji walilala kwa bao 1-0 na ushindi wa jana ulikuwa faraja kubwa kwa mashabiki wao.

Kama kawaida Mwanaspoti limefuatilia hatua kwa hatua mchezo huo na hapa linakupa tathimini ya wachezaji wa timu zote mbili walivyocheza na alama wanazostahili kupata. Alama ni kuanzia sifuri hadi 10 kwa kila mchezaji.