Yanga watibua sherehe Simba

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Simba, waliwasili Dar es Salaam, jana saa 2:40 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakiwa na kombe lao wakitokea Lindi walikotoa suluhu na Namungo FC.

Baada ya kuwasili walikaa ndani ya uwanja wa ndege kwa dakika 40, kukiwa na vikao vingi ambavyo havikuwa rasmi vilivyokuwa vikihusika kumtuliza kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck ambaye alionekana kuwa mkali na kuongea kwa sauti ya juu akiwa amekasirika. Sven hakutaka kuelewa lolote ambalo alikuwa akiambiwa na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda, wasaidizi wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji, na kuamua kutoka nje ya uwanja huku akiwa na hasira hata wengi wa mashabiki waliojitokeza kumshangilia na kumpigia makofi hakuwa na habari nao.

Baada ya kutoka Sven alimkaripia Msaidizi wa Ofisa mtendaji mkuu, Rispa Hatibu kwa nini aliweka utaratibu wa wachezaji kupanda gari la wazi, na kwa nini ameacha wingi wa mashabiki kuja uwanja wa ndege kuwapokea na kuishangilia timu hiyo jambo ambalo hakulitaka akitaka wachezaji wakapumzike kujiandaa na mechi ngumu ya Yanga, Jumapili.

“Sitaki kuona mchezaji yeyote anapanda katika gari la wazi na kuzunguka nalo, badala yake wote wapande basi la timu na kwenda kambini moja kwa moja,” alionekana Sven akimueleza Rispa kwa ukali na sauti ya juu ingawa naye alikuwa akiwasiliana na mabosi zake kuwaeleza juu ya hilo kwa njia ya simu.

“Sitaki jambo lolote lifanyike hapa, hakuna mchezaji wala msaidizi wangu yeyote kufuata utaratibu wowote ambao umepangwa hapa, na nimewakataza kuongea hata na vyombo vya habari, kwani tuna mechi ngumu ambayo tunahitaji utulivu tujipange kwa ushindi, hatuwezi kupoteza muda na nguvu,” alisikika Sven akiwaambia wenzake kwenye ‘mzozo’ huo.

Kwa upande wake, Rispa ambaye alikuwa akijibu huku kama machozi yakimlenga alieleza kuwa amefuata utaratibu ambao uliwekwa na uongozi na alikwenda uwanjani hapo kusimamia na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na ndio maana walikodi na magari. “Unanikaripia mbele ya watu ili iweje wakati ambacho nakifanya hapa na mambo mengine ni masuala ambayo yalipangwa na uongozi, ambalo nalifanya ni utekelezaji wa majukumu yangu,” Rispa alijibu kwa sauti kali, huku akirusha mikono na wenzake wakijaribu kumtuliza.

Baada ya mzozo huo Kocha msaidizi, Selemani Matola na Meneja Patrick Rweyemamu waliingilia mzozo huo na kuwatenganisha kila mmoja wakimpeleka upande wake ili kuepusha mzozo zaidi mbele ya mashabiki, madereva teksi, abiria na vyombo vya habari.

Baada ya hapo wachezaji walitoka ndani ya jengo ya uwanja na benchi la ufundi na kuingia katika gari ambazo zilifika kuwapokea na kwenda moja kwa moja kambini Mbweni kupitia Tazara, Buguruni, Ilala, Magomeni, Kinondoni kisha Moroco, Makumbusho, Mwenge, Tegeta hadi Mbweni. Walisindikizwa na Coaster tatu, gari ndogo tatu na bodaboda kadhaa huku wachezaji wakiwa wametulia kwenye gari kana kwamba hakuna kilichotokea.

Mwanaspoti liliwafuata Kaduguda, Sven, Matola na Rweyemamu kuzungumzia mkanganyiko uliotokea, lakini wote waligoma kuzungumzia suala hilo la kubadilishwa kwa ratiba ya tukio la Simba kusherehekea ubingwa wao na mashabiki.

Awali, mara baada ya mechi na Namungo kumalizika Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alieleza kuwa kikosi hicho kingewasili saa 3:30 asubuhi na baada ya hapo kingetumia gari la wazi ambalo lingewabeba wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na baadhi ya viongozi wakiwa na kombe kuzunguka mitaani kuelekea makao makuu ya timu yaliyopo Msimbazi, kisha ndipo wangeelekea kambini, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

WADAU WAFUNGUKA

Akizungumzia sintofahamu iliyotokea, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema: “Halikuwa jambo baya kutembea na kombe wakitokea uwanja wa ndege, lakini ni lazima uamuzi wa kocha uheshimiwe kwa sababu wachezaji wanatakiwa kuelekeza akili zao katika mchezo wa Yanga kuliko sherehe za ubingwa.”

Naye Ulimboka Mwakingwe ambaye aliwahi kutamba na Wekundu hao wa Msimbazi alisema: “Wangesema wafanye sherehe kwa kutembea mitaani ni wazi kuwa siku nzima ingeisha bila ya kufanya mazoezi na wachezaji kupumzika. Sherehe zinaweza kufanyika baadaye kwa sababu kuna mechi mbele za ligi.”

IMEANDIKWA THOBIAS SEBASTIAN, OLIVER ALBERT NA ELIYA SOLOMON