Yanga Princess yajipanga kimtindo

Kikosi cha Yanga Princess kikiwa kwenye picha ya pamoja kujindaa na moja ya mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) ambayo kwa sasa imesimama kupisha dirisha dogo la usajili.

ALIYEIPANDISHA Yanga Princess, Maalim Saleh na sasa anafanya majukumu mengine ya kuwa kocha msaidizi wa Serengeti Boys, amefichua kitu ambacho kilikuwa mwiba kwa timu hiyo kushindwa kufurukuta nafasi tatu za juu.

Saleh alisema licha ya kutoendelea kuinoa Yanga Princess amekuwa mshauri wa karibu na benchi la ufundi la timu hiyo kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani dhidi ya zile ambazo zinatikisa nafasi tatu za juu kama JKT Queens, Alliance na Mlandizi Queens.

Alifichua kwamba kikosi cha Yanga Princess kina wachezaji wengi ambao wana uwezo mdogo usiofaa kucheza kwenye ligi, jambo alilodai tayari ameongea na wale ambao wanatakiwa kusajiliwa.

“Kama nilivyosema nipo karibu kulishauri benchi la ufundi, nimezungumza na wachezaji sita na nimewakabidhi benchi la ufundi ili wakamilishe usajili, naamini wakiwafanikisha hao watakuja kivingine kwenye raundi ya pili.

“Kuna vitu vingi vilivyokuwa vinaifanya Yanga Princess kushindwa kuwa na matokeo ya uhakika ambavyo siwezi kuviweka wazi badala yake viongozi wanalifanyia kazi jambo hilo,”alisema.

Mwanaspoti liliwahi kumnukuu katibu mkuu wa Yanga, Omary Kaya akisema mchango wao kwenye timu hiyo ni kuhakikisha wanafanya usajili wa maana kupitia dirisha dogo.