Yahya Al Ghassani ajifunga miaka mitano Al Wahda

Muktasari:

Yahya amesaini mkataba wake wa kwanza kuwa mchezaji wa kulipwa kwenye klabu yake ya Al Wahda inayoshiriki Ligi Kuu Falme za Kiarabu

BWANA mdogo Charly Musonda ilimlazimu Oktoba 15, 2016, kusubiri kwa dakika 20 ili kuonana na Cristiano Ronaldo mara baada ya mchezo kati ya Real Betis na Real Madrid kumalizika kwenye uwanja wa Benito Villamarín.

Musonda ambaye alikuwa kwa mkopo Betis akitokea Chelsea hakutaka kupoteza nafasi hiyo na kuamua kutega ili kuonana na nyota huyo anayemkubali katika soka kwenye siku yake hiyo ya kuzaliwa.

Unaambia hakujali Musonda licha ya Betis kukumbana na kipigo cha mabao 6-1 alitimiza alicholenga kwa kuonana na Ronaldo pindi alipokuwa akiingia kwenye basi la Real Madrid akitokea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Wakati Musonda akimuangaikia Ronaldo, mambo ni tofauti kwa upande wa pili ambao unamhusu Mtanzania anayekichafua kwenye falme za Kiarabu, Yahya Al Ghassani.

Yahya mwenye umri wa miaka 20, hivi karibuni alipata nafasi ya kuisaini mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa kwenye klabu yake ya Al Wahda inayoshiriki Ligi Kuu kwenye falme hizo za Kiarabu.

Kusaini kwake mkataba wa miaka mitano kumemfanya atimize ndoto yake ya kucheza timu moja na nyota ambaye alikuwa akimhusudu kwa kupindi kirefu kwenye kikosi hicho.

Nyota huyo ambaye baba yake ni Mtanzania huku mama yake akiwa raia wa falme za Kiarabu, anasema wakati akichipukia kwenye soka la vijana alikuwa akivutiwa na staili ya uchezaji ya Ismail Matar ambaye kwa sasa soka lake linaishia.

Matar alitikisa kwenye soka la falme za Kiarabu kwa kushinda mataji sita akiwa na Al Wahda, matatu kati ya hayo ni ya Ligi Kuu ‘UAE’ nchini humo kwenye misimu ya 2000–01, 2004–05, 2009–10, mara mbili ni Super Cup kwenye miaka ya  =2002, 2011.

Huku akishinda mara moja kombe la Al Etihad "Union" mwaka 2001. Pia mshambuliaji huyo anashikilia tuzo nane tofauti kwenye uchezaji wake soka la ushindani.

“Wakati nachipukia ilikuwa ni ndoto yangu kuichezea Al Wahda, kila kitu kimekuwa wazi. Alikuwa ni zaidi ya rafiki kwangu kila nilipokuwa nikipata nafasin ya kuongea naye pindi nilipokuwa kikosi cha vijana.

“Baada ya kupanidishwa na kupewa mkataba huo mpya mwanzoni mwa msimu nilijisikia furaha kwa sababu niliona ndoto yangu inaenda kutimia ya kucheza pamoja na mchezaji ambaye nilikuwa nikitamai kuwa kama yeye,” anasema.

Moja ya mahojiano ya Matar na mtandao mkubwa nchini humo wa The national.ae/international aliwahi kumzungumzia kijana huyo wa Kitanzania na kusema ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu.

“Anapenda kujifunza na mara kadhaa amekuwa akipenda kuambiwa ukweli, anaweza kuja kuwa mchezaji mkubwa baadaye,” aliwahi kusema Matar.

Yahya baada ya kupandishwa kikosi cha kwanza, ameonekana kuwa na mwenendo mzuri kwa kufunga bao lake la kwanza la msimu kwenye Ligi katika mchezo wa Septemba 9 dhidi ya     Al Wasl.

Bao hilo, mshambuliaji huyo alifunga dakika ya 40 kwenye ushindi wa mabao 3-0 ambao waliupata wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Sheikh Zayed Sports City, Abu Dhabi.

Licha ya kupopata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, Yahya amekuwa akipata dakika chache na kuonyesha uwezo wake ambao umekuwa gumzo nchini humo.

Nyota huyo wa Kitanzania aliyeichezea Al Wahda michezo minne ya Ligi anatajwa kuwa moja ya makinda yanayochipukia kwa kasi kwenye taifa hilo la falme za Kiarabu.

Ndoto za kinda huyo wa Kitanzania ni kupiga hatua za zaidi ya nyota wake anayemhusudu kwenye soka Matar ambaye alikuwa akipachika mabao kila kukicha pindi ambapo damu yake ilikuwa ikichemka.

Yahya aliwahi kuweka wazi kuwa anatamani siku moja kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kwenye Ligi kubwa zenye ushindani ambazo zinaweza kumfanya kuwa mchezaji wa daraja la juu.

Tusubiri tuone muda unaweza kuongea kwa kinda huyo wa Kitanzania kama  atapiga hatua zaidi ya nyota wake ambaye anamkubali kwenye soka japo yeye mwenyewe anaamini Matar hakuwa na njaa ya kucheza soka kwenye Ligi kubwa Ulaya.

WASIFU WAKE

Jina Kamili; Yahya Al Ghassani

Kuzaliwa : Aprili 18, 1998

Umri: 20

Timu: Al Wahda

Nafasi: Mshambuliaji