Winga Yanga anukia Prisons

Winga machachari wa Yanga, Emmanuel Martin

Muktasari:

  • MKATABA wa winga machachari wa Yanga, Emmanuel Martin umesalia muda mchache na kumpa nafasi ya kuzungumza na klabu yoyote kwa sasa na tayari ameweka bayana anataka kuondoka Jangwani ili kupata timu mpya.

WINGA EMMANUEL Martin ambaye amegeuka ‘mtumishi hewa’ ndani ya Yanga kwa kutopewa nafasi na Kocha Mwinyi Zahera anajiandaa kuchomoka klabu hapo ili akatafute maisha Prisons Mbeya.

Martin ambaye katika mechi 10 za Yanga hajabahatika hata kukaa benchi na hilo ndilo linamchoma moyo na sasa anaamua kusema zake Jangwani.

Mkataba wake unaishia mwishoni mwa Desemba, lakini alisema anatamani kupata mahali za kuendeleza kipaji chake na anataka kutumia dirisha dogo huku ikielezwa Prisons tayari inampigia hesabu za kubeba.

“Nahitaji kucheza, ili nijiweke sokoni, kama Yanga itashindikana kubaki na kupata nafasi basi nahitaji timu itakayonipa nafasi ya kucheza,” alisema.

Hata hivyo, Katibu wa Prisons, Abdallah Havimtishi alifichua kuhitaji huduma za winga huyo akisisitiza ana kasi na nguvu ya kufosi mashambulizi na kwamba wakifanikisha kumsajili basi watakuwa wamepata jembe.