Wiki ya kituko cha Morrison, Mkude

Monday June 29 2020
Mkude pic

Wasalaam wapenzi wasomaji wangu. Leo sina jambo kubwa, lakini ni muhimu kulizungumzia ili kwenda pamoja. Wiki hii tulisikia adhabu iliyostahili kuchukuliwa mwezi Februari, ikitolewa Juni bila ya sababu za msingi, jambo linalokaribisha tuhuma bila ya sababu.

Jonas Mkude wa Simba na Bernard Morrison wa Yanga walihukumiwa kwa makosa ambayo kama wangetumikia adhabu, wiki hii wangekuwa walishasahau kama walifanya makosa yaliyostahili kuzuiwa kucheza mechi mbili.

Nashindwa kuelewaa kwa nini tunaenda mbele halafu tunarudi nyuma. Nadhani huko kwa kuchelewesha uamuzi tulishatoka zamani sana kiasi kwamba nilidhani wawili hao walishaonekana hawana hatia au kamati za TFF zilishindwa kupata ushahidi wa kuwatia hatiani.

Nilipouliza imekuwaje, nikaambiwa kwamba eti kamati ya nidhamu haikupelekewa shauri hilo kwa hiyo wa kulaumiwa ni sekretarieti. Nadhani hilo lilikuwa ni jibu na si jawabu. Jibu hilo halikulenga kuanika kiini cha tatizo na hivyo kuweka njia ya suluhisho.

Jibu ni rahisi kutoa lakini jawabu ni gumu kwa sababu linaeleza sababu ya tatizo na suluhisho lake.

TFF iliunda Kamati ya Saa 72—zamani Kamati ya Mashindano—ili iwe inapitia uamuzi wa refa na kuyaidhinisha na pale inapotokea mwamuzi hakuona tukio, basi kwa kutumia teknolojia waamue kwa niaba ya mwamuzi au kamati ya nidhamu kwa kuzingatia kanuni za nidhamu.

Advertisement

Ni wazi kuwa matukio ya uwanjani hayahitaji mkosaji kuitwa na kuulizwa sababu ya kufanya tukio fulani, bali kuadhibiwa na ndio maana hawa jamaa wanapewa mamlaka hayo ya kushughulikia kosa lililotokea ndani ya mchezo wakati umesimma na ambalo mwamuzi hakuliona.

Hili halisubiri Kamati ya Nidhamu ikae baada ya miezi mine. Ndio maana hata Kanuni za Nidhamu za Fifa zinaeleza matukio ambayo yanahitaji uamuzi wa haraka ambayo yanafanywa na jaji mmoja tu ili mambo yaendelee.

Haya matukio ni lazima yafanyiwe uamuzi haraka ili mkosaji aone machungu ya kosa lake kuliko aadhibiwe wakati amesahau kuwa aliwahi kufanya kosa.

Ndio maana adhabu ya Mkude haimuumizi kwa kuwa imetolewa wakati majeruhi na hivyo hawezi kuchezeshwa kwa sasa. Hata kwa Morrison adhabu haimuumizi sana kwa mazingira yaliyopo katika klabu hiyo kutokana na ukweli kwamba Yanga ilishaondoka katika kinyang’anyiro cha ubingwa.

Moja ya mambo yaliyoufanya mpira wa miguu uchukue mkondo wake wa kisheria katika masuala yanayohusu mchezo ni taratibu ndefu za mahakama wakati mpira unataka mambo yaamuliwe ili uendelee.

Kama kosa la Morrison lingetakiwa liamuliwe na mahakama kungekuwa na kasheshe nyingi. Kwanza kujenga hoja kwamba ana kesi ya kujibu, kukataa ushahidi uliowasilishwa, kutokamilika kwa upelelezi, kumuona kwamba ana kesi ya kujibu, kusikiliza mashahidi na mambo mengine mengi hadi mwaka kesho wakati hukumu itakapotoka. Na bado kama akikutwa na hatia, awe na siku 30 za kuijulisha mahakama nia ya kukata rufaa. Wakati kesi ikiendelea, upande mmoja ungeomba ligi isimamishwe hadi kesi kuu iishe. Duh!

Naeleza hayo nikitaka kuonyesha kuwa mpira uliyaona hayo na ndio maana ukaandaa vyombo vyake vya uamuzi ili tatizo likitokea liamuliwe mara moja.

Sasa tukianza kupuuza umuhimu wa kuwa na vyombo vya uamuzi na vikaamua kwa kasi inayohitajika ili mchezo uendelee, ni ngumu kusizuke hisia kuwa uamuzi umefanywa leo na si Februari kwa lengo la kuihujumu timu fulani.

Tusipofanya hivyo, atatokea mtu mmoja huko kwetu Tukuyu na kufungua kesi na hapohapo kuomba amri ya muda wa mahakama izuie ligi hadi suala la Morrison litakapotolewa uamuzi. Yalikuwepo hayo na tulishatoka huko. Sasa tumesahau tunataka hawa watu-- ambao wanajua kabisa kuwa hata wakifungiwa, hawaathirika—warejee tena kutunyoosha?

Suala la tukio la ndani ya dakika 90 au dakika chachw kabla na baadaye halihitaji Kamati ya Nidhamu yote, bali hiyo ya saa 72 ambayo inatakiwa ikae mara baada ya mechi za raundi moja nzima kumalizika na kuidhinisha adhabu za mwamuzi na kuadhibu zile ambazo angeziona angeadhibu kwa mujibu wa kanuni za nidhamu.

Kama Kamati ya Saa 72 haijapewa mamlaka hayo, ni wakati wa kuangalia upya suala hilo.

Advertisement