Wawa amkaribisha beki Mwamnyeto msimbazi

KATIKA eneo ambalo kocha wa Simba, Sven Vandenbroek ameshaweka wazi anataka kuongezea nguvu ni beki wa kati na ambaye anatajwa sana kwa hapa ndani ni Bakari Nondo Mwamnyeto kutokea Coastal Union ya Tanga.

Mwanaspoti ina taarifa kuwa mabosi wa Simba, wameingia sokoni kutafuta beki mwingine wa maana wa kigeni na wamefika mpaka katika timu za Zambia, DR Congo, Ghana na nchi nyingine. Beki wa kati wa Simba, Pascal Wawa ambaye mkataba wake na timu hiyo unafikia ukingoni mwisho wa msimu huu alieleza kuwa litakuwa jambo zuri kama atakuja beki mwingine wa kati kwani ataongeza hali ya ushindani katika eneo hilo.

“Nimecheza soka la ushindani kwa muda mrefu kwa maana hiyo kama atakuja beki wa kati mwingine kati yetu ambaye atafanya vizuri majukumu yake mazoezini na kwenye mechi ndio atapata nafasi ya kucheza,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Azam na El Merreikh ya Sudan.

“Binafsi si jambo la kushangaza kwangu kwani nafahamu kama nikifanya vizuri nitastahili kucheza lakini nikiona nipo chini nitastahili kuwa benchi jambo ambalo kwa sasa najiona sina nafasi ya hilo.

“Kwa hiyo sina wasiwasi na hili na niwakaribishe kwenye timu wachezaji wetu wapya ambao tutakuwa nao msimu ujao,” alisema Wawa.

Mwanaspoti inafahamu Simba watamuongezea mkataba wa mwaka mmoja Wawa lakini wanataka kuboresha katika eneo lao la beki wa kati kutokana wanaweza kuwapiga chini walinzi Yusuph Mlipili, Kennedy Juma na Mbrazil Tairone Santos.