Wamecheza mechi kibao bila kupoteza

Muktasari:

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City walianza msimu kwa ubora mkubwa wakitoa vichapo kwa timu zote zilizokatiza mbele yao na kuonyesha mapema tu inakwenda kutetea ubingwa wake.

LIGI Kuu England bado hakijaeleweka. Mbio za ubingwa ni Liverpool na Manchester City na hapo kila mtu ana nafasi ya kulibeba taji hilo.

Kwenye vita ya kumaliza ndani ya Top Four kumenoga zaidi. Tottenham Hotspur, Arsenal, Manchester United na Chelsea zote zina nafasi ya kuwapo kwenye orodha hiyo, ambayo inahitaji timu mbili tu baada ya Liverpool na Manchester City kuonekana kujichukulia nafasi mbili za mwanzo tayari.

Vuta nikuvute hiyo inayokana na vikosi vyote kufanya vizuri kwenye ligi hiyo kwa msimu huu baada ya kuona timu kibao katika kipindi fulani cha msimu zilicheza mechi kibao bila ya kupoteza na ndio maana ushindani umekuwa mkali.

Msimu huu umekuwa na timu nyingi zilizolinda viwango vyao kwa muda mrefu na ndio maana ushindani ni mkali.

Hii hapa ndio orodha ya timu zilizocheza mechi kibao bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England msimu huu zikiongozwa na Liverpool ambayo kwa sasa ndio wanaoshika usukani wa ligi hiyo licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi zaidi ya wapinzani wao kwenye mbio hizo, Man City.

5. Chelsea (mechi 12)
Chelsea ya Kocha Maurizio Sarri inapambana na hali yake kupenya kwenye Top Four ya Ligi Kuu England na kuwafanya watu kushangaa kuona kulikoni hasa baada ya timu hiyo kuwa na mwanzo mzuri sana wa msimu.

Kocha huyo Mtaliano alikuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi hiyo ambapo aliongoza Chelsea kucheza bila ya kupoteza kwenye mechi 12 za ligi.

Baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Manchester City katika Ngao ya Jamii, Chelsea iliingia kwenye Ligi Kuu England ikiwa na hasira na kucheza mechi 12 bila ya kupoteza, huku kwenye mechi hizo ilitoka na ushindi mara nane na kutoka sare nne.

Makali yake hayo ya kucheza bila ya kupoteza yalikwenda kumalizwa na Tottenham Hotspur baada ya kuichapa 3-1 katika mchezo wa ligi uliofanyika uwanjani Wembley.

4. Man United (mechi 12)

Miezi sita ya mwanzo ya majanga kwa Kocha Jose Mourinho katika msimu wake wa tatu katika kikosi cha Manchester United kilimshuhudia Mreno huyo akifungashiwa virago vyake na kufunguliwa mlango wa kutokea huko Old Trafford. Akaja Ole Gunnar Solskjaer, ambaye alihitajika kufanya maajabu kurudisha timu hiyo kwenye makali yake na hakika aliweza kulifanikiwa hilo.

Wachezaji wa kikosi hicho walionekana kumwelewa zaidi Kocha Ole, ambaye alikuwa mshambuliaji wa zamani kwenye kikosi hicho na baada ya hapo wakaanza kugawa dozi na kupoteza mechi tena kijinga. Man United ikacheza mechi 12 kwenye Ligi Kuu England bila ya kupoteza, huku mechi walizoshinda zikiwa 10 na kutoka sare mbili katika kipindi hicho walicheza bila ya kuonja machungu ya kupoteza mechi. Arsenal ndio iliyokuja kuvunja rekodi ya kutopoteza baada ya kuichapa 2-0 uwanjani Emirates.

3. Arsenal (mechi 14)

Baada ya kukumbana na vipigo viwili mfululizo katika mechi mbili za mwanzo wa msimu kutoka kwa Manchester City na Chelsea, Arsenal ilitulia chini ya kocha wake mpya, Unai Emery na kucheza mechi 14 zilizofuatia kwenye Ligi Kuu England bila ya kuonja machungu ya kupoteza.

Ilianza mchakamchaka wake wa kutopoteza mchezo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham United na baada ya hapo iliendelea kugawa dozi katika mechi sita mfululizo zilizofuatia. Katika mechi hizo 14 ilizocheza bila ya kupoteza, iliibuka na ushindi katika mechi 10 na kupata sare nne. Rekodi yake ya kutopoteza ilikuja kumalizwa na Southampton wakati Arsenal ilipoduwazwa kwa kipigo cha mabao 3-2.

2. Man City  (mechi 15)

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City walianza msimu kwa ubora mkubwa wakitoa vichapo kwa timu zote zilizokatiza mbele yao na kuonyesha mapema tu inakwenda kutetea ubingwa wake.

Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kilicheza mechi 15 bila ya kupoteza, kikishinda mara 13 katika mechi hizo na kutoka sare mbili, huku mechi tano kati ya hizo ilizoshinda tofauti ya mabao kwenye mechi ilikuwa matano. Mwendo wa Man City wa kutofungwa ulikuja kumalizwa na Chelsea, ambapo iliichapa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

1. Liverpool (mechi 20)

Liverpool ilifungua pochi kwenye madirisha ya usajili ya mwaka jana na hakika hilo limelipa. Kikosi hicho cha Kocha Jurgen Klopp kilianza msimu huu kwa gia kubwa na kuna kipindi hata iliwaacha kwa mbali wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa, Man City. Liverpool ilicheza mechi 20 bila ya kupoteza kati ya Agosti 12 hadi Januari 3, ikishinda 17 na kutoka sare tatu. Mwendo huo wa kutopoteza ulikuja kumalizwa na Man City, ilipoichapa 2-1 uwanjani Etihad. Tangu wakati huo, Liverpool haijapoteza tena kwenye ligi, ikicheza mechi 10. Kwa msimu huu, Liverpool ndio ilicheza mechi nyingi bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England.