Wamebeba mara nyingi tuzo ya mchezaji bora wa mechi msimu huu

Monday April 15 2019

 

LONDON,ENGLAND.KUTAJWA kuwa Mchezaji Bora wa Mechi hiyo inaonyesha ubora wa mchezaji husika katika mechi kwa maana ya kucheza kwa kiwango matata kuliko wengine wote.

Sasa kuna wachezaji hao imekuwa jambo la kawaida kwao kucheza kwa ubora mkubwa katika kila mechi na ndio maana wamejikuta wakichaguliwa mara nyingi sana kuwa wachezaji bora wa mechi kwenye ligi za huko Ulaya kwa msimu huu.

6. Daniel Parejo - mara 8

Daniel Parejo amekuwa kwenye kiwango bora kabisa akicheza kiungo ya kati kwenye kikosi cha Valencia msimu huu, akifunga mabao manane katika mechi 29 alizocheza.

Kiwango chake bora kimewafanya Valencia kuwa kwenye mchakamchaka wa kusaka soka la Ulaya kwa msimu ujao. Ubora wake wa uwanjani haujaachwa hivi hivi na ndio maana staa huyo amechaguliwa mara nane kuwa Mchezaji Bora wa Mechi na hakika anahitaji kucheza kwa ubora huo ili kutamba zaidi Ulaya.

5. Raheem Sterling - mara 8

Raheem Sterling anaipaisha Manchester City na amekuwa kwenye kikosi matata kabisa tangu Pep Guardiola alipotua huko Etihad. Sterling amekuwa mchezaji muhimu wa Man City katika mpango wao wa kubeba mataji manne msimu huu, akiwa amefunga mabao 19 katika mechi 42 alizocheza kwenye michuano yote.

Kiwango chake bora ndani ya uwanja kimemfanya Sterling achaguliwe Mchezaji Bora wa Mechi mara nane tofauti kwa msimu huu hadi sasa.

4. Cristiano Ronaldo - mara 9

Moja ya wachezaji mahiri kabisa katika historia ya mchezo wa soka ni Cristiano Ronaldo. Kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, staa huyo aliwaduwaza wengi alipoamua kuachana na Real Madrid na kwenda kujiunga na Juventus, mahali ambako ameendeleza moto wake mkali ndani ya uwanja.

Ronaldo na umri wake wa miaka 34 amefunga mabao 25 katika mechi 37 na kuchaguliwa mara tisa tofauti kuwa Mchezaji Bora wa Mechi kwenye ligi msimu huu.

3. Nicolas Pepe - mara 11

Sapraizi kubwa kabisa kwenye ligi za Ulaya msimu huu. Nicolas Pepe amekuwa kwenye ubora wake huko Lille msimu huu na kuwafanya kuwa moto akifunga mabao 19 katika mechi 33 alizocheza na kiwango hicho ndicho kinachoifanya timu yake anayocheza kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligue 1.

Pepe mwenye umri wa miaka 23 tu, ambaye amekuwa akiwindwa na vigogo kibao kwa msimu huu, amechaguliwa mara 11 tofauti kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.

2. Eden Hazard - mara 13

Baada ya kuboronga hapo kati, Chelsea wamerudi tena kwenye ile Top Four ya Ligi Kuu England shukrani kwa kazi nzuri kabisa ya staa wao, Eden Hazard.

Hakuna ubishi supastaa huyo wa Kibelgiji ndiye mchezaji wao bora kabisa kwa msimu huu akifunga mabao 19 hadi sasa, huku ubora wake wa ndani ya uwanja akiwa na uzi wa The Blues ukimsaidia kutajwa mara 13 kuwa Mchezaji Bora wa Mechi. Hazard akiondoka Stamford Bridge ataacha pengo kubwa kwelikweli.

1. Lionel Messi - mara 15

Mshindi mara tano wa Ballon d’Or, supastaa Lionel Messi ndiye kinara wa mabao kwenye mchakamchaka wa kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya msimu huu baada ya staa huyo kufunga mabao 43 katika mechi 41 za michuano yote aliyocheza.

Kiwango cha Messi huko Barcelona kimekuwa hakina shaka na ndio maana kwa msimu huu amechaguliwa mara 15 tofauti kuwa Mchezaji Bora wa Mechi. Messi ndiye moyo wa wababe hao wa Nou Camp akiwabeba kwa mbeleko.

Advertisement