Wachezaji waungana kuomboleza kifo cha mama Abdul

Muktasari:

Beki wa Yanga, Juma Abdul amefiwa na mama yake mzazi asubuhi ya leo yeye akiwa kambini Mwanza kwaajili ya kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Zesco.

NYOTA wa soka wameungana na Juma Abdul kuomboleza msiba mkubwa uliompata wa kumpoteza mama yake mzazi asubuhi ya leo Alhamisi.
Abdul akiwa Mwanza ambapo timu yake imeweka kambi kwaajili ya kujiandaa na mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco amepokea taarifa za kuondokewa na mzazi wake huyo.
Kwa nyakati tofauti wachezaji wa timu mbalimbali wametumia mitandao yao ya kijamii kumpa pole na kumtia moyo kwenye kipindi hiki kigumu anachokipitia.
Ibrahim Ajibu mshambuliaji wa Simba, kupitia ukurasa wake ameandika kuwa "Rafiki wa kweli ndugu yangu Juma Abdul pole sana kwa kuondokewa na mama mzazi faraja iwe nawe katika kipindi hiki kigumu.
Mchezaji wa Yanga, Deusi Kaseke ameandika "Pole sana kaka yangu kwa kumpoteza mama Mungu akupe uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kila nafsi itaonja umauti,".
Kipa namba tatu wa Yanga, Ramadhani Kabwili ameandika "pole sana kaka yangu Juma kwa kuondokewa na mama yako kipenzi,".
Beki wa zamani wa Yanga na sasa anakipiga Polisi Tanzania, Pato Ngonyani ameandika "Pole sana kaka Juma kwa kumpoteza mama, sote njia yetu ni moja tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu,".