Vitendo vya utekeji vyamtisha Joti

Muktasari:

  • Msanii wa maigizo Lucas  Mhuvile 'Joti' ana hofu na watu wasioujulikana ambao wameibuka nchini na kufanya vitendo vya utekaji. Matukio ya watu kutekwa yanawapa hofu na kuogopa hata magari yanayopita karibu yake.

MSANII wa vichekesho, Lucas Mhuvile’Joti’, amesema vitendo vya watu kuendelea kutekwa na watu wasiojulikana vinawatisha hata wao wasanii.

Joti ni kati ya wasanii waliounda kundi la vichekesho la Original Comedy lililokuwa na wasanii Mpoki, Masanja Mkandamizaji na Wakuvanga ambalo lilikuwa likirusha vichekesho vyake kituo cha EATV na baadaye kuhamia TBC.

Kwa sasa msanii huyo amekuwa akifanya kazi zake mwenyewe huku akisikika zaidi kwa jina la dada Kiboga, alisema vitendo hivyo vinawaweka katika wakati mgumu wasanii kutokana na kujulikana na watu wengi.

“Ndugu kama unavyoona watu wasiojuliana wanateka wanaojulikana, jambo hili kama wasanii linatupa hofu sana kwani sasa hivi ukiwa kwenye gari mtu akipita pembeni yako unaogopa.

“Tumekuwa tukitembea kwa hofu kwani kila ukiamka na ukifika sehemu yako ya kazi na kurudi salama, unashukuru Mungu mana hali imekuwa sio hali,’alisema Joti.

Hivi karibuni mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewji alitekwa na watu wasiojulikana katika Hoteli ya Collosseum.

Pamoja na familia yake kutangaza donge nono la Sh1 bilioni kwa mtu atakayeweza kutoa taarifa za alipo, bado hajapatikana..