Vigogo Arusha Utd kitanzini

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mnguto alisema walikuwa kwenye mchakato wa kukusanya malalamiko ya timu zote na kuyajadili ndani ya Kamati ya Saa 72, hivyo kitendo cha Arusha United kusema Bodi wamekosa weledi ni kuikosea kamati hiyo kwani malalamiko yao mengi yamefanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni ikiwemo dhidi ya Rhino Rangers huko Tabora.

BODI ya Ligi nchini huenda ikawaburuza kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) viongozi wa klabu ya Arusha United kuthibitisha kauli yao ya kuwakashifu kuwa wamekosa weledi katika uendeshaji wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni uongozi wa Arusha United kutangaza kujitoa kwenye ligi hiyo kwa kile walichodai kukosekana kwa weledi kwenye mashindano hayo, hasa bodi hiyo. Viongozi hao walidai Bodi ya Ligi imeshindwa kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo walivyoeleza kuwa ni vya kihuni walivyofanyiwa kwenye mechi zao za ugenini. Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mnguto alisema walikuwa kwenye mchakato wa kukusanya malalamiko ya timu zote na kuyajadili ndani ya Kamati ya Saa 72, hivyo kitendo cha Arusha United kusema Bodi wamekosa weledi ni kuikosea kamati hiyo kwani malalamiko yao mengi yamefanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni ikiwemo dhidi ya Rhino Rangers huko Tabora.

“Hao Arusha United walipanga kujitoa maana sijaona sababu za msingi, wao walileta barua yao hapa na timu zingine nyingi tu na leo (jana Ijumaa) tulipanga kamati ikae itoe uamuzi na kujadili barua zote sasa ninashangaa wakati tunashughulikia wao wanatangaza kujitoa na kutoa kauli mbaya kwetu na kashfa hiyo wakati sisi tuko kwa mujibu wa sheria”

Alizitaka timu zinazoona zinaonewa na waamuzi au wapinzani wapeleke malalamiko yao TFF na yatafanyiwa kazi kwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na sio kujitoa kwenye mashindano au kutishia kujitoa.