Vibaka wamliza Mahrez mamilioni

MANCHESTER, ENGLAND. DUH! Majanga. Winga staa wa Manchester City, Riyad Mahrez amevamiwa na wezi nyumbani kwake na kumtia hasara kwa kumwibia saa za thamani, pesa na vito vyenye thamani ya mamilioni.

Wezi hao wanaripotiwa kuingia nyumbani kwa staa huyo na kuiba saa tano, zinazotajwa kuwa na thamani ya Pauni 300,000 (sawa na zaidi ya Sh.850 milioni za Tanzania).

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ni kwamba miongoni mwa saa hizo, ipo ya brandi ya Richard Millie inayogharimu mkwanja mrefu wa Pauni 230,000 huku zile nyingine mbili, moja ni Rolex Daytona yenye thamani ya Pauni 40,000 na Rolex Day Date yenye thamani ya Pauni 35,000.

Sambamba na saa hizo, wezi hao pia waliiba pesa taslimu zaidi ya Pauni 50,000, vidani vya kuvaa mkononi na jezi orijino kabisa zenye thamani ya Pauni 150,000 na kumfanya Mahrez awe amelizwa na wezi hao kwa gharama za jumla za zaidi ya Pauni 500,000, ambayo ukichenji kwenye pesa ya Kitanzania ni zaidi ya Sh.1.4 bilioni.

Taarifa ya polisi ya Manchester ilibainisha: “Muda wa saa 11 jioni, Ijumaa ya Aprili 24, polisi walipigiwa simu wakipewa taarifa kwamba kuna uvamizi wa wezi katika moja ya makazi ya katikati ya jiji.”

Hili si tukio la kwanza kwa kipindi cha karibuni linalohusu mastaa wa Ligi Kuu England kuandamwa na wezi.

Mapema mwezi uliopita, kiungo wa Tottenham, Dele Alli alivaliwa na wezi wenye visu nyumbani kwake huko London, wakati mchezaji mwenzake Jan Vertonghen, familia yake ilivaliwa na wezi wakati yeye akiwa Leipzig kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Machi mwaka huu.

Mahrez amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu akifunga mabao saba na kuasisti manane kwenye Ligi Kuu England.