Utamu wa mziki LA Liga unaanza hivi

MADRID, HISPANIA. MCHAKAMCHAKA wa La Liga utamu wake utarudi Juni 11 kwa kushuhudiwa kipute cha Andalusian kabla ya vinara Barcelona kuingia mzigoni saa 48 baadaye.

Sevilla na Real Betis watakuwa na shughuli pevu kwenye mechi ya kwanza itakayopigwa Ramon Sanchez Pizjuan usiku huo wa Alhamisi. Baada ya hapo, Barca watasafiri kuwafuata Real Mallorca Jumamosi wakati watakapoingia uwanjani kulinda pengo lao la pointi mbili kileleni.

Mechi ya mwisho ya ugenini waliyocheza Barcelona kabla ya ligi kusimamishwa, walishinda 1-0 dhidi ya Real Sociedad baada ya kutokea kwenye kichapo cha el Clasico huko Bernabeu.

Real Madrid watacheza saa 24 baadaye baada ya mahasimu wao kucheza na wanaamini wataendeleza vita ya kufukuzia ubingwa watakapochuana na Eibar.

Los Blancos walibeba mara moja tu La Liga tangu 2012, mwaka 2017 walipokuwa chini ya Zinedine Zidane. Zaidi ya hapo wamekuwa wakiwashuhudia tu Barcelona wakitamba kwa kubeba mataji chini ya Ernesto Valverde.

Lakini, kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya Quique Setien, ambaye amekabidhiwa majukumu ya kuwania mataji matatu msimu huu. Bato hilo litashuhudia pia Sevilla waliopo kwenye nafasi ya tatu wakikipiga na Real Betis, wakati Valencia kwenye nafasi ya saba, wao watakipiga na Levante.

Sociedad waliopo kwenye nafasi ya nne watakuwa na shughuli mbele ya Osasuna katika mchezo wa mwisho wa wikiendi hiyo.

Atletico Madrid, ambao mechi yao ya mwisho kucheza kabla ya ligi kusimama ulikuwa ushindi wa mabao 3-2 uwanjani Anfield dhidi ya Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, watakuwa ugenini San Mames kukipiga na Athletic Bilbao.

Getafe watacheza na Granada katika moja ya mechi mbili zitakazopigwa Ijumaa usiku sambamba na ile ya Valencia na Levante.