Ushindi wa Yanga FA gumzo

Dar es Salaam. Ushindi wa Yanga wa mabao 2-1 juzi dhidi ya Kagera Sugar ulioiwezesha kuingia nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) umeibua gumzo.

Gumzo hilo linatokana na penalti ya iliyoamua mshindi huku baadhi ya mashabiki wakisema mwamuzi Shomari Lawi hakuwa sahihi.

Yanga ilitoka nyuma na kusawazisha kabla ya kuongeza bao la pili kwa penalti katika dakika ya 73 ya mchezo huo uliofanyika usiku kwenye Uwanja wa Taifa.

Kagera ilipata bao lake katika dakika ya 19 lililofungwa na Awesu Awesu ambaye katika dakika ya 79 alionyeshwa kadi ya pili ya njano hivyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Yanga ambayo sasa itachuana na mshindi wa mechi ya jana usiku kati ya Simba na Azam ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 52 kupitia kwa David Molinga kabla ya Deus Kaseke kufunga bao hilo la penalti baada ya Juma Nyosso kumchezea faulo Mrisho Ngassa.

“Haikuwa penalti halali kwa sababu faulo ilifanyika nje ya 18,” alisema nahodha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Ally Mayay.

Alisema kwa kuwa mwamuzi hakuwa na plani B, ndiyo sababu alitoa penalti.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na VAR kwa sababu kuna matukio yanaweza kumpita mwamuzi kwa bahati mbaya, ndiyo maana Wazungu waliona umuhimu wake.

Hata hivyo, alisema mwamuzi hatakiwi kukosea na ikiwa hivyo, iwe kwa kiwango cha chini.

Mwamuzi wa zamani wa kimataifa, Abdulkadir Omary alisema hakuridhishwa na mwamuzi wa mechi hiyo, “alifanya makosa mengi, sijapata usingizi jana ‘juzi’ kwa hasira, nawaza nini ambacho alifanya uwanjani, hivi sisi waamuzi ndiyo tunafanya vile? Kweli bado soka la Tanzania lina safari ndefu.”

Awali, mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Israel Nkongo alisema kitakachoweza kusaidia kupunguza makosa ya waamuzi nchini ni VAR.

“Waamuzi ni binadamu si malaika, hivyo nao wanakosea, ili kupunguza makosa ni kuwa na VAR, hakuna kingine,” alisema.

Makocha Yanga, Kagera

Wakati kocha Luc Eymael akiwapongeza wachezaji wake kwa kiwango bora katika mchezo huo hasa kipindi cha pili, Mecky Maxime wa Kagera Sugar alisema walichofanyiwa wanamuachia Mungu.

Alisema hawana cha kufanya kwa namna mwamuzi alivyowafanyia katika mchezo huo kwani soka la Tanzania ndivyo lilivyo.

“Kila mmoja ameona mechi ilivyokuwa, tumefungwa ni sawa, tumekubaliana na matokeo kwani soka letu ndivyo lilivyo, mengine tunamwachia Mungu,” alisema Maxime akiwa njiani na timu yake kurejea Kagera.

Kocha Luc aliipongeza Kagera kwa upinzani iliouonyesha huku akifafanua kuwa bao ambalo timu yake ilifungwa ni makosa ya kipa Metacha Mnata.

“Bao hilo ni kama tulilofungwa kwenye mechi na Biashara, Metacha alipaswa kurudi hatua chache upande wa kushoto kisha anyooshe mkono kuutoa mpira uliokuwa unaelekea golini, hakufanya hivyo,” alisema.

Alisema amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake hasa kipindi cha pili japo kuna makosa madogo ya kuyafanyia kazi.

“Tunahitaji kufanya vizuri zaidi na kuwa bingwa wa FA ili tushiriki mashindano ya kimataifa, tunajua tutacheza nusu fainali na Azam au Simba, yoyote kati yao tunamsubiri, bahati nzuri timu zote tunazifahamu, hivyo tunajipanga.”

Akizungumzia kadi alizopewa, Awesu alidai kuwa hajui sababu, kwani hata kadi ya kwanza alishangaa ilikuwaje.

“Kadi ya pili nilichezewa faulo, mchezaji mwenzangu alipaniki hivyo nikachukua jukumu la kumtuliza ghafla nashangaa nakutana na kadi nyingine sijui ilikuaje, sijaongea jambo lolote na wala sijatukana aulizwe hata refa mwenyewe,” alisema.