Upelelezi wakwamisha kesi ya Wambura

Friday March 15 2019

By FORTUNE FRANCIS

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, umedai upelelezi haujakamilika na uko katika hatua nzuri.

Wakili wa Serikali Wankyo Saimon alidai jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Kelvin Mhina, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

“Mheshimiwa kesi hii imekuja ili itajwe, upelekezi haujakamilika lakini umeshafikia hatua nzuri tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa,” alidai Wakili Wankyo.

Baada ya Hakimu Mhina kusikiliza maelezo hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 28 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa na mshtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh100 milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbalimbali na riba kutoka kwa Kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadaiwa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF na kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh10 milioni kutoka TFF kwa kuonyesha ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh25 milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.

Advertisement