Unai amkalisha chini Ozil

Muktasari:

Katika mazungumzo ya Unai na Ozil, kocha huyo alimweleza kiungo huyo kuwa Arsenal inamtegemea kufanya vizuri katika dimba la kati ili kusaidia kusukuma mbele mashambulizi, lakini haiwezi kupata ushindi kirahisi bila eneo analocheza kuwa na ufanisi.

KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amemkalisha kitako nyota wake, Mesut Ozil kisha akatoka na uamuzia wa kumpa muda upya ili ajitafakari kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya England kabla hajafanya uamuzi mweingine wa kuachana naye.
Licha ya Unai kuzungumza naye kwa muda mrefu, inafahamika kwamba wamiliki wa Arsenal wanasikilizia ofa kutoka katika timu mbalimbali zilizoonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo ili waweze kuachana naye katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, ni timu moja pekee ya Fenerbahce ya Uturuki ambayo imeonyesha nia ya kumchukua mchezaji huyo mwenye asili ya nchi hiyo, lakini aliye na uraia wa Ujerumani pia, ingawa zipo taarifa kwamba inataka apunguze mshahara wake anaolipwa Arsenal ili iweze kumsajili.
Ndani ya Washika Bunduki hao wa London, Ozil analipwa mshahara wa Pauni350,000 kwa wiki kiwango ambacho Waturuki hao wenzake hawawezi kukimudu kumlipa kwa wiki.
Katika mazungumzo ya Unai na Ozil, kocha huyo alimweleza kiungo huyo kuwa Arsenal inamtegemea kufanya vizuri katika dimba la kati ili kusaidia kusukuma mbele mashambulizi, lakini haiwezi kupata ushindi kirahisi bila eneo analocheza kuwa na ufanisi.
Unai amemwambia Ozil asipojipanga na kufanya vizuri dimbani, basi hatakuwa na namna nyingine ya kumsaidia zaidi ya kumpiga benchi na msimu wa dirisha dogo ataushauri uongozi kuachana naye hata kama itakuwa na kumlipa gharama za mkataba wake uliosalia ili aende zake.
Mashabiki wa Arsenal hawataki kumuona mchezaji huyo ambaye tangu alipotua Arsenal akitokea Real Madrid kiwango chake kimekuwa kikipanda na kushuka, lakini aliwashangaza wengi alipokabidhiwa mkataba mnono na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger miezi michache kabla hajatimuliza.
Ozil, 30, amekuwa akitupiwa lawama na mashabiki wa timu hiyo wakimlaumu muda mwingi kucheza chini ya kiwango, ambapo timu hiyo imekuwa ikiwategemea zaidi washambuliaji wake, Pierre Emerick Aubameyang na Alexander Lacazete kusaidia eneo la kiungo anachoza huku pia wakiwa na jukumu la kufunga mabao.