Ujanja wa Samatta, Mrundi aushtukia, ammwagia sifa

Muktasari:

  • SOKA alilopiga Mbwana Samatta katika mechi ya kuwania tiketi ya Afcon 2019 kati ya Tanzania na Cape Verde yamemfanya Kocha Mrundi, Ramadhani Nsuzurwino kufichua kuwa, madini aliyolishwa staa huyo wa kimataifa wa Tanzania ndiyo chanzo cha kuwa mkali kisoka na kutaka wengine wafuate mkumbo huo.

KOCHA mwenye uraia wa nchini mbili za Burundi na Afrika Kusini, Ramadhani Nsanzurwino amemuangalia straika na nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta na kufichua siri ambayo hata baadhi ya mashabiki wa soka huenda hawakuwa wanajua.

Kocha huyo alisema staa huyo wa Genk ya Ubelgiji, amedhihirisha yeye ni mfano wa kuigwa kwa taifa lake, lakini alisema kinachomfanya Samatta atishe ni kucheza kwake nje ya nchi na kulishwa ‘madini’ ya kizungu yanayomfanya ajitofautishe na wenzake.

“Licha ya kukosa penalti, alicheza vizuri akatoa pasi ya goli na akafunga.” Alicheza vizuri jambo ambalo hata kwa wachezaji wadogo wanaomwona wanahamasika kutokana na mabadiliko ya kila siku anayoonyesha,”alisema Nsanzurwino.

“Kuna mabadiliko makubwa kwake kila siku na hii inaonyesha ni kwa namna gani kucheza nje kuna vitu vingi vya kujifunza na ndicho anachokifanya Samatta, ni wazi kutoka kwake nje na kufanya kazi Ulaya kumejenga kisoka,” alisema Nsanzurwino. Samatta ambaye hakucheza soka Tanzania kwa kipindi kirefu baada ya kupata ‘dili’ TP Mazembe alikocheza kwa kipindi cha misimu mitano amewateka Wazungu anakocheza kiasi cha kufikia kumtungia wimbo, kitu ambacho amewahi kufanyiwa Mohammed Salah kwa mashabiki wa Liverpool.

Kwa sasa klabu mbalimbali za England zimeanza kumwania ili ajiunge kwao kama Everton na West Ham.

Samatta aliyekosa penalti mapema, lakini tukio hilo halikumtoa mchezo na badala yake kupambana na kuisaidia Stars kushinda mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde ndani ya Stars ni bwana mipango.

Kwani katika pambano hilo la majuzi alitengeneza bao la kwanza lililofungwa na Saimon Msuva kabla ya kufunga mwenyewe bao la pili lililoifanya timu ya taifa kufufua tumaini la kwenda Cameroon katika fainali za Afcon 2019 kutoka Kundi L.