Ubingwa wa Liverpool wainyima raha Man United

Manchester, England. Ubingwa wa Liverpool unaonekana kuipasua kichwa Manchester United.

Ni miaka tangu Liverpool ilipotwaa taji la England lakini mashabiki na mabosi wa Man United hawakupenda hilo litokee kwa mahasimu wao wakubwa.

Bado wanakuna vichwa kusuka upya kikosi cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer ili msimu ujao kuingia kwenye ushindani wa kuwania taji hilo na sio kushiriki na kuwa wasindikizaji.

Ili kuongeza ushindani na kuingia kwenye mbio za ubingwa, Manchester United bado inaisaka saini ya winga wa Borrusia Dortmund, Jadon Sancho (pichani).

Dortmund imeweka bayana kwamba inaweza kumuweka sokoni fundi huyo wa Kiingereza kama kuna timu itaweka mezani Pauni 110 milioni.

Kwenye orodha ya mastaa wapya wanaotakiwa na Solskjaer, jina lake ni la kwanza na ili kufanikisha mpango huo, Man United imekuja na mkakati mpya wa kuwapiga bei Alexis Sanchez na nyota wengine watatu ili kupata fedha hizo.

Inaamini kwamba imekuwa ikifuatilia maendeleo ya Sancho kwa zaidi ya misimu miwili sasa na sasa inamuona kama mtu sahihi wa kuongeza nguvu kwenye kikosi chake.

Habari za kuanimika zinaeleza kwamba Solskjaer amemwambia makamu mwenyekiti wake, Ed Woodward atafute mkwanja kwa ajili ya kukamilisha dili la Sancho kwenye dirisha lijalo la usajili.

Hata hivyo, mara kadhaa Ed aliwahi kukaririwa akieleza kwamba, janga la virusi vya corona limetibua uchumi wa klabu hiyo hivyo, hawatarajii kufanya uhamisho wa fedha nyingi.

Mastaa ambao wanaweza kuwekwa sokoni ili kuvuna kitita cha kupunguza bili za mishahara mbali na Sanchez anayelipwa Pauni 400,000 kwa wiki ni Jesse Lingard, Andreas Pereira na mabeki Phil Jones na Chris Smalling aliyepo AS Roma ya Italia kwa mkopo.