Ubingwa Gor Mahia waibua mjadala

Monday May 4 2020

 

By Eliya Solomon, Mwananchi esolomon@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Gor Mahia kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, wachezaji wa Tanzania wanaocheza mashindano hayo wamekuwa na mtazamo tofauti.

Ligi Kuu Kenya (KPL) imehitimishwa (uamuzi wa mezani) huku Gor Mahia anayocheza David Kissu na Dickson Ambundo wakitangazwa mabingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2019/2020.

Gor Mahia wametangazwa mabingwa wakiwa na pointi 54 baada ya mechi 23, huku kukiwa hakuna matumaini ya ligi kuendelea kutokana na uwepo wa ugonjwa wa covid-19.

Kissu ambaye ni kipa namba moja Gor Mahia, alisema;” Tumetangazwa kuwa mabingwa lakini hakuna mchezaji mwenye morali kwa sababu ya janga ambalo lipo mbele yetu.

“Ingependeza kama tungechukua ubingwa baada ya kumalizika msimu. Huu ni ubingwa wangu wa kwanza wa Ligi Kuu Kenya kwa muda ambao nimecheza nimejifunza mengi,” alisema.

Kipa Kabali Faraji aliyewahi kucheza Simba na African Sports ya Tanga ambaye kwa sasa anacheza Nzoia Sugar ya Kenya, alisema uamuzi ambao umefanywa na shirikisho hilo umeziumiza klabu za Kakamega Home Boys na Tusker.

Advertisement

“Kakamega wapo nafasi ya pili na Tusker ya tatu walikuwa na uwezo wa kuishusha Gor. Binafsi ni bora wangesubiri pindi ambapo hali ingekuwa shwari halafu msimu tukamalizia,” alisema kipa huyo ambaye timu yake ipo nafasi ya 15 kati ya timu 18.

Beki wa Kariobang Sharks, Aman Kyatta alifurahishwa na uamuzi huo huku akisema afya za mashabiki na wachezaji kwa ujumla ni bora kuliko kitu kingine.

“Kulingana na hali tuliyonayo ni maamuzi mazuri sana maana wameangalia kwanza utu,” alisema beki huyo ambaye timu yake ipo nafasi ya 12 katika msimamo wa KPL. Kissu, Ambundo na Kyatta walirejea nchini mapema kabla ya kufungwa kwa mipaka nchini Kenya. Faraj amebaki Kenya. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliandika barua Jumanne wiki iliyopita kujua uamuzi wa ligi husika kwa kila nchi.

Advertisement