‘Tunawapiga Simba tupate mzuka’

Muktasari:

Mechi ya mwisho kukutana na Simba, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0

BEKI na nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul amesema lazima washinde dhidi ya Biashara United na Kagera Sugar ugenini ili wapate mzuka wa kumchapa Mnyama Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Baada ya michezo hiyo timu hiyo itarejea Dar es Salaam kukipiga na Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na Abdul alisema licha ya kwamba, wanataka kumaliza ligi katika nafasi ya pili, lakini ushindi dhidi ya Simba ni muhimu zaidi kwao.

“Tumejiandaa vizuri kushinda mechi zetu zilizobaki kwani, tunataka kuona tunaimiliki nafasi tuliyopo sasa kwenye msimamo hadi mwishoni mwa msimu.

“Pia, tunataka kufika fainali ya FA na kubeba ubingwa kwani hiyo ndiyo nafasi pekee ambayo tumebakiwa nayo ya kutuwezesha kushiriki mashindano ya kimataifa hivyo, hatuwezi kukubali kuipoteza.

“Malengo yetu ni kuona tunashinda michezo miwili ya ligi, dhidi ya Biashara na Kagera kwani ushindi huo utatupa kasi ya kuikabili vizuri Simba,” alisema Abdul.