Tunamfikiria Adel Zrane pale Simba?

KWENYE benchi la ufundi la Simba kuna mtu mmoja raia wa Tunisia anayeitwa Adel Zrane. Huyu ni mtaalamu wa mazoezi ya viungo na kuweka fiti mwili.

Ana leseni ya juu ya ukocha kwenye eneo hilo inayotambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Ulaya (UEFA) lakini ana elimu ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya masuala ya viungo na lishe.

Alianza kuitumikia Simba mwanzoni mwa msimu pindi ilipokuwa kwenye kambi ya maandalizi kule Uturuki baada ya kupendekezwa na Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ambaye wakati huo ndiyo alikuwa anaanza kazi akirithi mikoba ya Pierre Lechantre.

Jukumu lake kuu ndani ya Simba ni kuhakikisha wachezaji wa timu hiyo wanakuwa fiti muda wote wa msimu ili waweze kumudu mfumo na mbinu za benchi la ufundi kwenye mechi za mashindano mbalimbali wanazoshiriki.

Ndiye ambaye amekuwa akiandaa na kusimamia programu zote za kujenga stamina, pumzi na ufiti kwa wachezaji lakini pia amekuwa ndiyo msimamizi mkuu wa masuala ya lishe kwa wachezaji wa Simba.

Mbali na hayo, Zrane amekuwa akikusanya video za kila mechi ambayo Simba inacheza kisha kuzituma kwenye jopo la wataalamu wa viungo lililopo Ujerumani ambalo humrudishia ripoti ya ufanisi wa mchezaji mmojammoja kikosini ambayo amekuwa akiitumia kuwaimarisha nyota wa Simba kwenye mchezo unaofuata.

Katika kipindi kama hiki ukikaa chini na kutafakari ndiyo utagundua faida ya kuwa na wataalamu wabobezi kama Zrane kwenye benchi la ufundi mbali na uwepo wa kocha mkuu.

Katika ratiba ngumu ya kucheza mechi nane za Ligi Kuu ambapo kati ya hizo sita ni ugenini nje ya Dar ambako kuna umbali mrefu huku muda wa kupumzika ukiwa mfupi chini ya saa 48, Simba imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Kagera Sugar.

Hapana shaka kwamba Zrane ametimiza majukumu yake vizuri na amewajengea vyema wachezaji wa Simba, ufiti na stamina hadi wakaweza kupata matokeo kwenye mechi hizo zilizoonekana awali kuwa wangepoteza kutokana na kutopata muda wa kutosha kupumzika.

Ni shujaa asiyeimbwa lakini anachangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kazi ya Aussems na benchi lake la ufundi kuonekana rahisi na nyepesi kutokana na jinsi anavyotimiza vyema majukumu yake pale.

Kwa nini Zrane hapewi sifa? Jibu ni rahisi tu kwamba mfumo wa soka la kisasa, huyu na wenzake wote wanawajibika kwa kocha mkuu au meneja wa timu kulingana na mfumo wake wa uendeshaji ulivyo.

Kuna timu ambazo mamlaka ya mwisho ya kiufundi yanakuwa kwa kocha mkuu lakini kuna timu nyingine ambazo mamlaka ya kiufundi yanaunganishwa na baadhi ya kiutawala yahusuyo benchi la ufundi na wachezaji ambayo yote yanaachiwa mikononi mwa mtu mmoja anayeitwa meneja.

Kwa soka la Tanzania, mkuu wa benchi la ufundi anaitwa Kocha Mkuu kwa sababu mara kwa mara anahusika na masuala ya ufundi tu lakini kwa nchi nyingi, timu zinakuwa na meneja kwa maana ya kocha anayekuwa na majukumu mengi zaidi ya yale ya ufundi.

Adel Zrane ni ishara tosha ya maana ya kuwa na benchi pana la ufundi kwa sababu linapunguza majukumu kwa kocha mkuu ambaye atapata muda wa kutosha kushughulikia masuala ya mbinu na kuandaa mpango wa mechi huku majukumu mengine yakibakia kwa jopo la makocha na wataalamu anaofanya nao kazi. Kwa bahati mbaya ukiondoa Simba, hakuna klabu nyingine nchini ambayo ina mtaalamu wa kama Zrane na ndiyo maana hivi sasa tunaona utofauti mkubwa.

Ni vyema tukamtumia Zrane kama chachu ya mabadliko kwenye klabu zetu na kuzishawishi ziajiri wataalamu sahihi na wa kutosha kwenye mabenchi yao ya ufundi kwani mfumo wa soka la kisasa unataka hivyo.

Hatuwezi kufanikiwa kimataifa kama tuna mabenchi ya ufundi yenye watu saba au sita. Wenzetu mabenchi yao ya ufundi yana watu hadi 40. Tuamke usingizini.