Taifa Stars kumenoga

Muktasari:

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amesema rekodi za nyuma hazipaswi kupewa nafasi kubwa kwenye mchezo wao na Uganda  kwani utakuwa na sura ya kitofauti.

DAKIKA 45 za kipindi cha kwanza zimeshikilia hatma ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mchezo wake muhimu wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Na kwa mzuka uliopo kwa sasa ndani ya Stars, huenda kazi ikaisha mapema sana.

Namna Stars itakavyozichanga karata zake vizuri katika muda huo, inaweza kuamua uwezekano wa kuibuka na ushindi, kutoka sare au kupoteza pambano hilo. Tathmini ya mechi za nyuma ambazo timu hizo zimecheza kuwania kufuzu Afcon zinazilazimisha safu za ulinzi na ushambuliaji za Stars kucheza kwa umakini wa hali ya juu kwani ndio muda ambao imekuwa ikifunga mabao lakini pia ndio wakati inaoruhusu nyavu zake kutikiswa mara kwa mara. Lakini pia ndio wakati ambao Uganda imekuwa ikiutumia zaidi kufunga mabao yake kama ilivyofanya kwenye mechi zake tano zilizopita.

Katika kudhihirisha hilo, katika mabao matatu ambayo Stars imefunga hadi sasa kundi hilo L, mawili iliyapata kipindi cha kwanza na moja tu ndio ilifunga kipindi cha pili na hasa katika dakika 30 za mwanzo.

Katika ushindi wa mabao 2-0 ambao iliupata dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 mwaka jana, bao la kwanza lilifungwa mnamo dakika ya 29 na Saimon Msuva na la pili lilifungwa na Mbwana Samatta katika dakika ya 57.

Bao lingine moja kati ya hayo matatu ni lile ambalo Stars ililipata katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho jijini Dar es Salaam ambalo lilifungwa na Samatta mnamo dakika ya 28.

Lakini, pia nyavu za Stars zimekuwa rahisi kutikisika katika kipindi hicho cha kwanza kwani katika sare ya 1-1 dhidi ya Lesotho, bao la wapinzani lilifungwa dakika ya 36, na kwenye kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde ugenini, mabao mawili yalifungwa kipindi cha kwanza dakika za 16 na 23.

Lakini Uganda ambayo hadi sasa haijaruhusu bao katika mashindano hayo, imefunga mabao manne katika kipindi cha kwanza huku matatu ikiyapata kipindi cha pili. Katika hali ya kushangaza mabao hayo yamekuwa yakifungwa zaidi katika dakika 30 za mwanzoni.

Kiungo mshambuliaji wa Uganda anayechezea HK Gorica ya Croatia, Farouk Miya ndiye anapaswa kuchungwa zaidi kwani ndiye amekuwa kinara wa ufungaji wa timu hiyo na amehusika katika mabao manne, akifunga matatu na kupiga pasi moja ya bao.

Hata hivyo, kocha wa Stars, Emmanuel Amunike alisema rekodi za nyuma hazipaswi kupewa nafasi kubwa kwenye mchezo huo kwani utakuwa na sura ya kitofauti.

“Mazingira ya mchezo huu ni tofauti na iliyopita. Ni mechi iliyoshikilia ndoto zetu ambazo tunapaswa kuamini kuwa ziko hai.

Wachezaji wanatambua wajibu wao kwa timu na pamoja na kwamba Uganda ni bora na yenye wachezaji wazuri, naamini vijana watapambana kuipa heshima.

“Wito wangu kwa mashabiki ni kuisapoti timu kwani hii ni nafasi ya kujenga historia kama nchi,” alisema Amunike ambaye amepewa jukumu moja zito la kuivusha timu kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1980 Fainali za Lagos, Nigeria.