TP Lindanda yawapigia hesabu Arusha Utd

Muktasari:

  • Ni mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza utakaopigwa jumamosi ya wiki hii jijini Arusha ambapo Kocha wa Pamba FC,Juma Yusuph Sumbu amesema wanataka ushindi ili kuongoza kundi B

LIGI  Daraja la Kwanza inatarajia kuendelea wikiendi hii ambapo Pamba FC  itakuwa mkoani Arusha kukipiga dhidi ya Arusha United, lakini kocha wa timu hiyo Juma Yusuph  amesisitiza kuwa ushindi wa ugenini ni muhimu kwani utawafanya waongoze Ligi.
Timu hiyo ya jijini Mwanza ndio kinara kwenye kundi lao B baada ya kuvuna pointi 11 sawa na wapinzani wao hao wakiwa na tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo baina ya timu hizo unatarajia kuwa mgumu kutokana na kila upande kuonyesha ushindani mkubwa na kuhitaji pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri kwenye vita ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Yusuph alisema baada ya sare yao dhidi ya Geita Gold wiki iliyopita kwa sasa wanajiwinda vikali kuhakikisha mchezo wa Jumamosi dhidi ya Arusha United wanashinda.
Alisema vijana wake wanaendelea vizuri na wana ari na morali na kwamba wanachohitaji katika mpambano huo ni pointi tatu ili kuendelea kujikita kileleni kwenye msimamo kundi B.
“Ni mchezo muhimu sana kwetu, haijarishi tupo ugenini au nyumbani, hii ni Ligi kwahiyo tumejipanga na tunaendelea kujifua kuhakikisha tunashinda na kubaki nafasi nzuri kwenye msimamo”alisema
Kocha huyo aliongeza kuwa licha ya kuwaamini nyota wake kuwa watafanya kweli lakini watawakabili wapinzani kwa tahadhari kubwa kwani mpira hautabiriki hivyo umakini lazima uzingatiwe.
“Mpira ukifanya makosa madogo unafungwa, pamoja na kuwaamini wachezaji wangu ila lazima tuwe makini na wapinzani wetu nitawaandaa kisaikolojia ili kutimiza malengo yetu,”alisema Kocha huyo.