Sven: Kuhusu Kagere mniache

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck amefunguka kuwa hana tatizo lolote na mshambuliaji Medie Kagere, lakini amesisitiza kuwa hatokuwa tayari kupangiwa kikosi na mtu yeyote.

Kauli hiyo ya Sven imekuja katika muda ambao kumekuwa na mjadala juu ya kitendo chake cha kumuweka benchi, Kagere, ambaye ndiye mfungaji Bora wa Simba na Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo iliyopita.

Lakini pia kocha huyo amekuwa akilaumiwa kwa kupendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao huwa unatumia mshambuliaji mmoja tu wa kati, jambo ambalo baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakiukosoa kuwa unachangia kuinyima timu hiyo ushindi.

Akizungumza jana, Vandenbroeck alisema kelele zinazopigwa juu ya Kagere na mfumo wake anazisikia, lakini hazimpi presha na ataendelea kusimamia anachokiamini.

“Suala la Medie Kagere ni la ndani ya timu. Kama kuna kasoro yoyote ya kiufundi, mimi kocha na Kagere mwenyewe tutaitatua na watu wa nje haliwahusu, hivyo sioni haja ya kulizungumzia.

“Kuhusu mfumo niseme tu kuwa ya watu lazima yawepo inaweza kuwa kutumia mfumo wa 4-4-2 au 4-3-3 lakini mwisho wa siku sisi tunafanya kile tunachoamini kuwa ni bora kwa upande wetu na sio vinginevyo,” alisema Vandenbroeck.

Hivi karibuni, meneja wa Kagere, Patrick Gakumba alinukuliwa na vyombo vya habari akimtuhumu Vandenbroeck kwa kutompa nafasi mshambuliaji huyo katika kikosi cha kwanza akidai kuwa kocha huyo hamtendei haki mchezaji wake.