Straika wa Simba arudishwa hospitali

Muktasari:

Abdul alikuwa pacha wa Yohana Mkomola katika kikosi cha Serengeti Boys kilichocheza Fainali za Afcon (Undr 17) nchini Gabon 2017.

STRAIKA Abdul Suleiman wa Simba ameondoka leo Ijumaa pamoja na kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' kilichokwenda kwa ajili ya kambi ya wiki mbili kabla ya kuanza michuano ya Fainali za Afrika 'Afcon' nchini Misri ingawa yeye amekwenda kutibiwa.
Abdul hayupo katika kikosi cha Amunike lakini ameongozana nao kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya baada ya kupata majeruhi alipokuwa na timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 18 kilichoshiriki mashindano maalumu hivi karibuni, Misri.
Abdul aliunga na Stars leo Ijumaa asubuhi wakati kikosi hicho kinafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuanza safari yao mchana ndipo alipoelezea juu ya safari yake hiyo.
"Nimekuja kuungana na timu kubwa maana naenda tena hospitali kulekule Misri, nilivunjika mkono, waliniambia nirudi tena kwaajili ya kuangaliwa," alisema.
Stars inajiandaa na michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 21 mwaka huu ambapo imepangwa Kundi C pamoja na timu za Senegal, Algeria na Kenya.